June 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanasiasa washauriwa kujikita kwenye masuala ya maendeleo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Tanga

WANASIASA hapa nchini,wameshauriwa kujikita katika masuala ya maendeleo ya wananchi badala ya kuanza kampeni za kutafuta urais wa mwaka 2030 wakati ni miezi sita tangu Serikali ya sasa iingie madarakani.

Kauli hiyo imetolewa jana na aliyekuwa mgombea wa nafasi ya kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Doyo,
Doyo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga baada ya kuhitimisha ziara yake ya kisiasa mkoani humo.

Doyo ameeleza kuwa, ingawa kila Mtanzania anayekidhi vigezo vya kisheria ana haki ya kuwania nafasi yoyote ya uongozi,jambo la kushangaza ni kuona baadhi ya wanasiasa kutoka chama tawala wakianza kuzungumzia urais wa mwaka 2030,kipindi kifupi baada ya uchaguzi mkuu kumalizika na Serikali mpya kuanza kazi.

“Ni miezi sita tu tangu Rais aapishwe na kuanza kutekeleza majukumu yake. Bado taifa lina safari ndefu katika awamu hii ya uongozi, lakini tayari kuna baadhi ya wanasiasa wanaotoa kauli zinazoashiria kutamani urais wa mwaka 2030. Hili si jambo lenye afya kwa maendeleo ya taifa letu,”amesema Doyo.

Amesema jukumu kubwa la viongozi waliopewa dhamana na wananchi kwa sasa ni kuhakikisha wanasimamia sera, mipango na mijadala itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, badala ya kuelekeza nguvu katika harakati za kisiasa za uchaguzi ambao bado uko mbali.

Kwa mujibu wa Doyo,Wabunge na viongozi wengine wa chama tawala wanapaswa kutumia nafasi walizonazo kuishauri na kuisimamia Serikali kupitia Bunge,ili kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya maendeleo yanayotarajiwa, badala ya kutumia majukwaa ya mijadala ya kitaifa kutangaza nia ya kuwania urais.

Pia amesema hali ya viongozi kuibuka katika mijadala ya bajeti au masuala mengine muhimu ya kitaifa na kuanza kuzungumzia urais wa mwaka 2030, inaondoa umakini katika hoja za msingi zinazohusu maisha ya wananchi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

“Tunahitaji mijadala yenye afya inayolenga kutatua changamoto za wananchi. Kiongozi anapokuwa na mawazo ya urais muda wote, kuna hatari ya kupoteza mwelekeo wa kushughulikia matatizo ya msingi yanayowakabili Watanzania,”amesisitiza.

Hivyo alitoa wito kwa wanasiasa wa vyama vyote hapa nchini,kutumia kipindi hiki kushirikiana kusukuma mbele agenda za maendeleo, badala ya kuingia katika ushindani wa kisiasa wa mapema ambao unaweza kuathiri umoja na mshikamano wa kitaifa.

Ameonya kuwa endapo hali hiyo itaendelea, inaweza kudhorotesha usimamizi wa masuala muhimu ya maendeleo na kuhamisha mjadala wa taifa kutoka kwenye utatuzi wa changamoto za wananchi kwenda kwenye siasa za urithi wa madaraka.

“Tunawaomba Watanzania kutambua kuwa kwa sasa taifa linahitaji viongozi wanaotatua kero za wananchi badala ya kujijengea mazingira ya kisiasa kwa ajili ya uchaguzi ujao. Kipaumbele kiwe maendeleo ya wananchi na si mbio za urais ambazo muda wake bado haujafika,” alisema.

Kwa upande wake MWenyekiti wa NLD Wilaya ya Tanga,Abdul Karney ameeleza kuwa wananchi wa Mkoa wa Tanga bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara katika maeneo kadhaa pamoja na uhaba wa maji kwa baadhi ya wilaya, hali inayohitaji juhudi za viongozi katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

Amesema wananchi wanatarajia kuona viongozi wakisimamia masuala ya maendeleo na utatuzi wa kero zinazowagusa moja kwa moja, badala ya kujihusisha na mijadala ya urais wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika miaka kadhaa ijayo.