Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Tanga,
SERIKALI imezitaka taasisi za elimu ya juu hapa nchini kuimarisha huduma za ushauri nasaha, malezi na ufuatiliaji wa wanafunzi ili kukabiliana na ongezeko la changamoto za afya ya akili, hususani msongo wa mawazo ambao umeendelea kuwaathiri vijana wengi waliopo vyuoni.
Wito huo umetolewa wakati ambapo wataalamu wa ushauri nasaha kutoka vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini, walipokutana jijini Tanga kujadili hali ya afya ya akili kwa wanafunzi, changamoto zinazowakabili pamoja na mbinu za kuimarisha huduma za msaada wa kisaikolojia katika taasisi za elimu ya juu.

Ambapo kwa mujibu wa washiriki wa mkutano huo,wameeleza kuwa changamoto za afya ya akili zimezidi kuongezeka kwa wanafunzi wengi wa vyuo vikuu,zinazosabanishwa na shinikizo la masomo, changamoto za kifedha, mabadiliko ya mazingira ya maisha, migogoro ya kifamilia pamoja na matarajio makubwa ya kufaulu katika elimu na maisha kwa ujumla.
Imeelezwa kuwa baadhi ya wanafunzi hushindwa kuhimili hali hiyo na kuingia katika msongo wa mawazo unaoweza kuathiri utendaji wao wa kitaaluma, uhusiano wao wa kijamii na hata afya zao kwa ujumla huku wengine wakilazimika kusitisha masomo.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo maalumu kwa washauri kutoka vyuo mbalimbali nchini, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Badru Abdunuru, amesema taasisi za elimu ya juu zinapaswa kutambua kuwa afya ya akili ni sehemu muhimu ya maendeleo ya mwanafunzi na haiwezi kutenganishwa na mafanikio ya kitaaluma.
Amesema mazingira ya sasa yanahitaji vyuo kuwekeza zaidi katika huduma za ushauri nasaha, kuajiri wataalamu wenye ujuzi wa kutosha na kuhakikisha wanafunzi wanapata msaada wa haraka wanapokumbana na changamoto za kisaikolojia.
Aidha, amesisitiza kuwa kuongezeka kwa visa vya msongo wa mawazo miongoni mwa vijana ni jambo linalohitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali, zikiwemo familia, taasisi za elimu, viongozi wa dini na wadau wa maendeleo ya vijana katika kutatua changamoto hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TACOGA 1984, Sophia Nchimbi, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wataalamu wa ushauri nasaha,ili waweze kukabiliana na changamoto mpya zinazoendelea kujitokeza katika mazingira ya elimu ya juu.
Ameeleza kuwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia, matumizi ya mitandao ya kijamii na ongezeko la changamoto za kijamii na kiuchumi,hivyo wataalamu wa ushauri wanapaswa kuendelea kujifunza mbinu mpya za kuwasaidia wanafunzi kwa ufanisi zaidi.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Nelson Mandela,Analyce Ichwekeleza amesema,mafunzo hayo yamewapa washiriki nafasi ya kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora za utoaji huduma na kuimarisha mtandao wa ushirikiano kati ya vyuo mbalimbali nchini.
Wataalamu hao wamehimiza kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya vyuo vikuu, washauri nasaha, wazazi, Serikali na wadau wengine wa elimu katika kuandaa programu za uelimishaji na kinga dhidi ya matatizo ya afya ya akili.



More Stories
Tucta kuzindua kituo cha msaada kwa wafanyakazi wahamiaji Juni 11
Wanasiasa washauriwa kujikita kwenye masuala ya maendeleo
Baraza la Tiba asili lafuta dawa zilizokiuka taratibu