Na Joyce Kasiki,Dodoma
NAIBU Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM) anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Jefta Sunzu, anesema Maonesho ya Nanenane yamekuwa fursa muhimu kwa UDOM kuwaonesha wananchi kazi zinazofanywa na wahadhiri na wanafunzi zinazoenda kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari katika vanda la USOM kwenye maobyeaho hayo Nzuguni jijini Dodoma ,Profesa Sunzu amesema , miongoni mwa bunifu zinazooneshwa katika maonesho hayo ni dawa zinazotokana na tafiti za ndani, bidhaa zinazolenga kuboresha lishe na afya, pamoja na teknolojia mbalimbali zinazolenga kurahisisha maisha ya wananchi.
Profesa Sunzu alisema chuo hicho pia kimewasilisha mifumo mbalimbali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), ambayo inaweza kutumika na Serikali pamoja na sekta nyingine kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
“Maonesho haya yanatupa nafasi ya kuwaonesha Watanzania kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma si mahali pa kufundisha tu, bali ni kitovu cha tafiti, ubunifu na teknolojia zinazotoa suluhisho la changamoto mbalimbali za jamii na kuchochea maendeleo ya Taifa,” alisema Profesa Sunzu.
UDOM yaandaa programu mpya
Profesa Sunzu pia alisema UDOM inaendelea kuboresha programu zake za masomo ili kuhakikisha inazalisha wataalamu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya Taifa na mabadiliko ya kiteknolojia yanayotokea duniani.
Alisema baadhi ya mitaala ya programu hizo tayari imewasilishwa katika Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya hatua zinazofuata, huku mingine ikiwa imeidhinishwa na kuanza kupokea wanafunzi..
Kwa mujibu wa Profesa Sunzu, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa UDOM kuendelea kuwekeza katika programu zinazozingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya Taifa, hususan katika kipindi ambacho sayansi, teknolojia na matumizi ya akili bandia vinaendelea kukua kwa kasi.
Aliwataka wazazi na walezi nchini kutumia fursa hiyo kuwapeleka watoto wao UDOM, akisema chuo hicho kinaendelea kuandaa programu zinazolenga kuwajengea vijana maarifa na ujuzi utakaowawezesha kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Alisisitiza kuwa uwekezaji katika elimu, tafiti na ubunifu ni muhimu katika kuandaa kizazi cha wataalamu wenye uwezo wa kutumia sayansi na teknolojia kutatua changamoto za jamii na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe Jabir Omary ambaye alitembelea banda la chuo hicho amekipongeza Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kuendelea kuzalisha tafiti na bunifu zinazolenga kutatua changamoto za wananchi katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, afya, usafirishaji na teknolojia.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea banda la UDOM katika Maonesho ya Nanenane katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, ambapo alieleza kuridhishwa na maendeleo ya chuo hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007.
Alisema ziara hiyo imempa fursa ya kujionea bunifu mbalimbali zinazofanywa na wahadhiri na wanafunzi wa UDOM, zikiwemo dawa zinazotokana na tafiti za ndani, mafuta asilia yasiyo na kemikali, teknolojia ya kutambua kiwango cha unyevunyevu wa udongo kwa ajili ya kurahisisha umwagiliaji, pamoja na mfumo wa White Box unaokusanya taarifa muhimu kuhusu ajali za magari kwa ajili ya uchunguzi.
Alisema mafanikio ya UDOM katika tafiti, ubunifu na mashindano ya teknolojia ndani na nje ya nchi yanaonesha mchango mkubwa wa chuo hicho katika maendeleo ya kisayansi, kiteknolojia na kijamii nchini.
Mkuu huyo wa Mkoa pia alieleza kuwa yeye ni miongoni mwa wanafunzi wa mwanzo wa UDOM, akisema elimu na malezi ya uongozi aliyoyapata chuoni hapo yamechangia kwa kiasi kikubwa katika safari yake ya utumishi wa umma hadi kufikia nafasi ya Mkuu wa Mkoa.
Aliwataka wazazi na walezi kuwahamasisha vijana kuchagua UDOM kwa ajili ya masomo ya juu, akisisitiza kuwa chuo hicho kinawajengea wanafunzi maarifa ya kitaaluma, maadili na uwezo wa uongozi unaoweza kuwawezesha kutimiza malengo yao.
Aidha, aliwashukuru viongozi, wahadhiri na watafiti wa UDOM kwa kuendelea kufanya tafiti na kuzalisha bunifu zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

More Stories
Busokelo yajipanga kumaliza udumavu
EWURA yaonya wanaofanya biashara bila leseni
Wakulima wapewa mbinu kukabiliana na Sumukuvu