June 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baraza la Tiba asili lafuta dawa zilizokiuka taratibu

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOnline,Dodoma

BARAZA la Tiba Asili na Tiba Mbadala limebaini dawa zenye mapungufu katika vifungashio,taarifa za lebo,ujazo,dozi na muda wa matumizi katika mwaka wa fedha 2025/26 na kuchukua hatua za kuondolewa sokoni mara moja,mtengenezaji akitakiwa kuzingatia taratibu bora za uzalishaji wa dawa asili hasa katika kipengele cha ukaushaji na uhifadhi.

Baraza hilo lilibaini hayo lilipofanya zoezi maalum  la ufuatiliaji wa dawa za tiba asili zilizopo sokoni katika mikoa ya Dodoma,Morogoro,Pwani na Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Juni 5,2026 ,kuhusu huduma za  tiba asili na tiba mbadala Mwenyekiti wa Baraza hilo Prof.Nicolao Otieno amesema kuwa katiza zoezi hilo dawa moja inayoitwa Joy ilibainika kuwa na sumu kuvu kwa kiwango kisichokubalika,hali iliyoashiria kutozingatiwa kwa viwango  bora vya uzalishaji wa dawa asili hususan wakati wa ukaushaji na uhifadhiwa dawa ghafi na dawa zilizokamilika.

“Kama inavyofahamika sumu kuvu ni hatari kwa afya ya binadamu na inaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo saratani ya ini,uharibifu wa figo,kupungua kwa kinga ya mwili pamoja na madhara mengine ya muda mrefu,”amesema Prof.Otieno.

Aidha ametaja dawa zilizobainika kuwa zimechanganywa na kemikali za dawa za kisasa zisizoruhusiwa ambazo hazikuainishwa kwenye lebo wala wakati wa usajili.

“Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa baadhi ya dawa za tiba asili zimechakachuliwa kwa kuongezewa dawa za kisasa kinyume cha sheria.Hali hii ni hatari kwa afya ya jamii na ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu na sheria zinazosimamia huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini,”amesema.

Prof.Otieno ametaja dawa hizo kuwa ni Powaful Banana Medicine ambayo ilibadilishwa kuitwa Banana Medicine inayotumika kama dawa ya kuongeza nguvu za kiume.

“Uchunguzi wa Maabara umeonesha kuwa dawa hiyo imechanganywa na kemikali za dawa za kisasa za kuongeza nguvu za kiume ambazo ni Slidenafil na Tadalafi pamoja na dawa za maumivu aina ya Tramadol na Paracetamol .Dawa hiyo imesajiliwa na Baraza na hutengenezwa na Kampuni ya Powaful Products Company Ltd,”amesema.

Ametaja dawa nyingine iliyobainika ni Vitamax(maarufu kama viasali)ambayo haijasajiliwa lakkni imekuwa ikitumika katika jamii kwa ajili ya kuongeza nguvu za kiume.

Prof.Otieno ameeleza kuwa kemikali hizo za dawa za kisasa ndani ya dawa za tiba asili bila usimamizi wa kitaalamu unaweza kusababisha madhara makubwa kwa watumiaji.

Amesema madhara hayo ni pamoja na matatizo ya moyo,figo,ini,shinikizo la damu,utegemezi wa dawa pamoja na hatari ya vifo kwa baadhi ya watumiaji.

Kutokana na hayo Baraza limesisitiza kuwa kitendo cha kuchanganya dawa za kisasa katika dawa za asili bila idhini ya Mamlaka husika ni kosa kinyume cha sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala sura 244 pamoja na kanuni za Maadili,mwenendo na utendaji za Tiba Asili na Tiba Mbadala za mwaka 2008 kifungu cha 18(d).