June 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tucta kuzindua kituo cha msaada kwa wafanyakazi wahamiaji Juni 11

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Evaline Munisi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Kituo cha Msaada kwa Wafanyakazi Wahamiaji Tanzania (TUCTA-MWRC) utakaofanyika Juni 11, 2026 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Rehema Ludanga, amesema uzinduzi huo utafanyika katika jengo la WDC lililopo Barabara ya Lumumba, Dar es Salaam.

Amesema kituo hicho kimeanzishwa kwa lengo la kuimarisha uratibu wa masuala ya uhamaji wa wafanyakazi na kuhakikisha Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi wanatumia njia salama, rasmi na zinazotambuliwa kisheria.

Ludanga amesema TUCTA, kama sauti ya wafanyakazi nchini, imeanzisha kituo hicho ili kutoa taarifa sahihi, ushauri na mwongozo kwa wafanyakazi wanaotafuta ajira nje ya nchi pamoja na wageni wanaokuja kufanya kazi Tanzania.

“Kituo hiki kitasaidia kuhakikisha haki, maslahi na ustawi wa wafanyakazi wahamiaji vinalindwa kupitia mikataba ya ajira iliyo wazi na inayozingatia maslahi yao,” amesema Ludanga.

Ameongeza kuwa mbali na huduma za ushauri, kituo hicho kitatoa mafunzo ya muda mfupi yatakayowawezesha wafanyakazi kujiandaa kwa mazingira ya kazi na maisha katika nchi wanazokwenda kufanya kazi.

Kwa mujibu wa Ludanga, hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa wafanyakazi kunufaika na fursa za ajira za kimataifa kwa usalama, ufanisi na tija zaidi.

Aidha, wafanyakazi wa kigeni wanaokuja kufanya kazi nchini watapata fursa ya kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kuhakikisha haki zao za msingi, maslahi na ustawi wao vinasimamiwa na kulindwa ipasavyo.