May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa elimu watakiwa kutoa maoni Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu

Na Irene Clemence, TimesMajira,Online, Dar

KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo, ametoa wito kwa wadau wa elimu kuendelea kutoa maoni katika hatua mbalimbali za maandalizi ya Mpango wa tatu wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu ili kuongeza wigo na ubora wa elimu inayotolewa kwa Watanzania.

Ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam jana wakati akifungua kikao cha wadau wa maendeleo ya sekta ya elimu wakati wakijadili taarifa ya uchambuzi wa hali halisi ya sekta ya elimu kwa mustakabali wa uimarishaji wa Sekta.

Amesema Wizara ipo katika uandaaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (2021/22 – 2025/26), hivyo ni vizuri kufanya uchambuzi wa hali halisi ya sekta katika kipindi cha utekelezaji wa mpango uliomalizika ili kujua yale yaliyopangwa yamefanikiwa kwa kiasi gani.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza katika mkutano huo Jijini Dar es Salaam jana.

“Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu Awamu ya Pili (2016/17 – 2020/21) umemalizika, hivyo uandaaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (2021/22- 2025/26) umeanza na hatua ya kwanza ni kufanya tathmini ya hali halisi ya sekta katika kipindi cha utekelezaji wa mapngo uliomalizika muda wake. Kazi hiyo ya kufanya uchambuzi ndio iliyotukusanya hapa leo hivyo nawaomba mtoe mapendekezo yenu katika ya namna ya kuboresha sekta ya elimu nchini,” amesema Katibu Mkuu Akwilapo

Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wadau katika kuwahudumia Watanzania wote kwa kutoa elimu bora katika ngazi zote, kuanzia elimu ya awali hadi Chuo kikuu na kwamba Wizara itaendelea kushirikiana nao kwa karibu na kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuharakisha azma ya Serikali ya kuleta maendeleo kwa wananchi

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mtaa TAMISEMI, Gerald Mweli akizungumza na wadau wa Elimu kutoka Taasisi mbalimbali binafsi na Serikali

Katibu Mkuu Akwilapo ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadau ambao wamegharamia zoezi la uchambuzi wa hali ya sekta ya elimu hapa nchini, ambao ni Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza, Benki ya Dunia na UNICEF ambao wamekuwa wasimizi Wakuu wa zoezi zima la tathmini ya sekta. Pia amewapongeza Washauri Elekezi, kitaifa na kimataifa waliotekeleza zoezi la uchambuzi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Fedha na Mipango.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Gerald Mweli, amesema majadiliano ya kikao hicho yanatoa mwelekeo wa namna ya kuboresha utoaji wa elimu nchini kwa kuchambua mafanikio na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mpango unaoisha.

Amesema TAMISEMI imepewa jukumu la kusimamia utoaji wa elimu msingi na sekondari nchini na kwamba kwa mwaka huu wa fedha wamefanikiwa kuajiri walimu 14,949 wanaofundisha elimu ya msingi na sekondari ikiwa ni sambamba na ujenzi wa miundombinu ili kuhakikisha ufundishaji unaendelea katika mazingira yaliyoimarishwa.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania, Lydia Wilbard ameonesha furaha yake kwa Serikali kufanya kikao hicho na kuwashirikisha wadau ambapo amesema ni utaratibu mzuri ndani ya serikali katika kuhakikisha kwamba Sekta ya elimu inapojadiliwa inahusisha wadau wa elimu kwani utekelezaji wa mipango ni jumuishi

Baadhi ya wadau walioshiriki katika mkutano huo ambao unafanyika kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam.

“Kushirikishwa kwetu sisi wadau tunapata fursa ya kuona kwa undani sekta yetu elimu imekwendaje na kutusaidia kupanga mikakati maalum ambayo italeta matokeo chanya katika kupanga mkakati unaokuja,”alisema Lydia Makamu Mwenyekiti Bodi ya TENMET.