May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SAGCOT kushirikiana na TADB kuongeza thamani ya mazao

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

VIONGOZI wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (Sagcot) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Nchini (TADB) jana wamekubaliana kuwa na ushirikiano katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi hapa nchini.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Sagcot, Geoffrey Kirenga, amewaeleza waandishi wa habari juu ya makubaliano hayo mara baada ya mkutano kati ya watendaji wa Sagcot na TADB uliofanyika kwenye makao makuu ya Sagcot, Masasani Peninsula, jijini hapa.

Ujumbe wa TADB umeongozwa na Mkurugenzi Mtendaji mpya, Frank Nyabundege, aliyeteuliwa mwezi jana na Rais Samia Hassan kuongoza benki hiyo.

“Tunaamini kwenye mabadiliko ya uongozi huwa kuna nguvu mpya ya kiutendaji hivyo tutashirikiana na TADB katika kufanya mageuzi katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi hapa nchini,” alisema Kirenga na kueleza kuwa ujumbe wao uliipata nafasi ya kumweleza Mkururgenzi wa TADB namna Sagcot inavyofanya kazi na kuwa kuna haja ya kutengeneza ubia ambao utasaidia kukuza na kuendelea kilimo nchini kwa kuhakikisha mahitaji ya mkulima yanafikiwa ili kukifanya kilimo kuwa endelevu.

“Jukumu letu kubwa ni kuhakikisha wawekezaji katika sekta ya kilimo wanatambuliwa na wanatoa mchango kwenye mahitaji ya wakulima wadogo nchini. Tunaamini kwa kushirikiana na TADB tutaongeza ufanisi katika eneo hili,” amesema Kirenga

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege (Watatu kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Menejimenti ya Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT) hivi karibuni alipotembelea na kujitambulisha kwenye ofisi za Kituo hichi jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa SGCOT, Geoffrey Kirenga. Picha na Paul Mahundi.

Alisema kuna uhitaji mkubwa wa kifedha ili kuwawezesha wakulima kuendesha kilimo bora na chenye tija. Hivyo wadau kama Sagcot na TADB wana wajibu wa kutoa elimu kwa wakulima juu ya kuzifikia taasisi za kifedha zilizopo namna ya kupata mikopo.

“Tanzania ina nafasi kubwa ya kufanya mageuzi katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kutokana na jiografia yake, na kuzalisha mazao mengi kwa soko ndani na nje ya nchi,” amesema Kirenga

Amefafanua kuwa kuna haja ya kuunganisha nguvu ili malengo ya kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi yafanikiwe na nchi iweze kuingia katika uchumi wa viwanda ifikapo 2025.

“Tutawaunganisha TADB na wadau wa Sagcot ili kuongeza nguvu katika kuhakikisha mahitaji ya wakulima yanawafikia kwa wakati na kukiendeleza kilimo,” amesema Kirenga

Nyabundege ameshukuru Sagcot kwa mapokezi mazuri na kusema kuwa mwongozo waliopata kutoka Sagcot utaiwezesha benki yao kuendeleza kwa urahisi na haraka juhudi za kuwasaidia wakulima na kukifanya kilimo kuwa cha kibiashara nchini.

“Ushirikiano kati yetu na Sagcot utatuwezesha kuwafikia wakulima wengi zaidi katika maeneo tofauti nchini na kupelekea uzalishaji kuongeza,” amesema Nyabundege.