August 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi watakiwa kutunza,kulinda barabara

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

WAKALA wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Mwanza,imesema asilimia 26.5 ya mtandao wa barabara unaousimamia bado upo katika hali isiyoridhisha kutokana na changamoto mbalimbali, zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la mtandao wa barabara na uharibifu wa miundombinu.

Kutokana na hali hiyo akizungumza na Majira ofisini kwake,Meneja wa TARURA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Makori Kisare,ametoa wito kwa wananchi na viongozi wa mitaa na kata kushirikiana kulinda miundombinu ya barabara, kuheshimu hifadhi za barabara.

Pia kuepuka kutupa taka kwenye mitaro na kukemea vitendo vya wizi ili fedha ambazo wanatumia kukarabati na kurejesha samani za barabara bazo zimeibwa zielekezwa kwenye ujenzi na matengenezo ya barabara badala ya kurejesha miundombinu iliyoharibiwa.

Mhandisi Kisare amesema,hadi Juni 30, 2026, mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 8,586 ulikuwa na kilomita 2,024 sawa na asilimia 23.6 zilizo katika hali nzuri, kilomita 4,288 sawa na asilimia 49.9 katika hali ya kuridhisha na kilomita 2,273 sawa na asilimia 26.5 katika hali isiyoridhisha.

Amesema,sehemu kubwa ya barabara hizo ambazo zipo katika hali ya kutoridhisha hupitika wakati wa kiangazi pekee, huku nyingine zikiwa ni barabara mpya ambazo bado hazijafanyiwa matengenezo.

Ameeleza kuwa,mabadiliko ya tabianchi yameongeza mvua kubwa zinazoharibu madaraja, makalvati na barabara nyingi, hususani miundombinu ya zamani ambayo haikujengwa kwa usanifu unaokidhi mahitaji ya sasa.

Aidha amesema,baadhi ya barabara wamezirithi kutoka halmashauri wakati TARURA ilipoanzishwa mwaka 2017, huku nyingine zilijengwa bila kufanyiwa usanifu wa kitaalamu na hivyo kushindwa kuhimili ongezeko la maji.

Kwa mujibu wake, vijijini wananchi wamekuwa wakilima ndani ya hifadhi za barabara na kuziba mifereji ya kupitisha maji, hali inayochangia kuharibika kwa barabara.

Sanjari na hayo amesema,katika maeneo ya mijini changamoto kubwa ni wizi wa miundombinu ikiwemo alama za barabarani,nguzo na hivi sasa kuna wimbi la wizi wa betri za taa za barabarani, jambo linalolazimisha TARURA kutumia fedha za matengenezo kurejesha vifaa hivyo.

Pia amesema,mahitaji ya barabara yanaendelea kuongezeka kila mwaka kutokana na ukuaji wa miji na kufunguliwa kwa barabara mpya, wakati bajeti haiongezeki kwa kasi inayolingana na mahitaji hayo.