April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jinsi wachambuzi wanavyomuelewa Mzee Mwinyi

Na David John

Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili Mzee Alli Hassan Mwinyi Jan amesherekea siku yake ya kuzaliwa ambapo amefikisha miaka 95 huku akiwa na afya Njema kabisa.

Kutokana na kufikisha umri huo kwa nyakati tofauti wakizungumza na Majira,watanzania wa kada mbalimbali wamempongeza mzee Mwinyi kwa kufikisha umri huo huku wakiendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumpa afya njema na maisha marefu.

Mzee Mwinyi ambaye ameliongoza Taifa la Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Pili amebaki kuwa Rais mwenye kupendwa na kukumbukwa na hasa kutokana na ile kauli yake maarufu ya Ruksa ambayo ilifungua fursa ya maendeleo kwa watanzania walio wengi.

Wakati leo Mzee Mwinyi ametimiza miaka 95 tangu kuzaliwa kwake ni vema tukakumbushana japo kwa ufupi historia yake.

Mzee Mwinyi alizaliwa Mei 8 mwaka 1925 kisiwani Unguja huko Zanzibar na alikuwa Rais kuanzia mwaka 1985 mpaka mwaka 1995.

Rais huyo mstaafu alipokea kijiti cha urais kutoka kwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza na Baba wa Taifa la Tanzania Hayati Mwalimu Julius Nyerere.Hata hivyo Mzee Mwinyi naye alikabidhi kijiti cha urais kwa Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu mzee Benjamin Mkapa.

Historia ya Mzee Mwinyi inaonesha mbali ya kuwahi kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya pili,pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kuanzia mwaka mwaka 1990 hadi mwaka 1996.

Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya siasa na uchumi kwa nyakati tofauti kwenye maandiko yao mbalimbali baadhi yao wanaeleza kuwa wakati wa urais wa Mwinyi, sera za Ujamaa zilianza kugeuzwa na kukawa na sera za soko huria ambapo masharti ya kuingiza bidhaa kutoka nchi za nje yalipunguzwa na uanzishaji wa biashara ya watu binafsi ulihamasishwa.

Mwaka wa 1991, uanzishaji wa vyama vingi uliruhusiwa.Hata hivyo inaelezwa kupitia historia yake kuwa kabla ya hapo alikuwa Rais wa Tatu wa Zanzibar kuanzia mwaka 1984 hadi 1985.

Aliyemtangulia ni Aboud Jumbe Mwinyi na aliyemfuatia ni Idris AbdulWakil Nombe.

Pia kabla hajachaguliwa kuwa Rais, Mzee Mwinyi maarufu kwa jina la Mzee Ruksa alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Makamu wa Rais na kuna wakati aliamua kujiuzulu nafasi hiyo na kisha kukaa kando lakini nyota yake iliibuka na kung’aa kiasi cha kuwa Rai katika Serikali ya Awamu ya Pili.

Mzee Mwinyi licha ya kuwa na umri mkubwa bado ameendelea kuwa na afya njema na amekuwa mstari wa mbele katika kufanya mazoezi na kwanyakati tofauti amekuwa akishiriki mbio mbalimbali ambazo zimekuwa zikiandaliwa na wadau mbalinbali.

Pia uwepo wake na hasa kwa kuzingatia uzoefu wa kuongoza nchi,Mzee Mwinyi ameendelea kuwa.moja ya viongozi ambao Taifa la Tanzania linamtegemea katika kushauri na kutoa maelekezo kuhusu mambo mbalimbali pale ambapo anafuatwa kuombwa ushauri na viongozi waliopo madarakani.

Baada ya kupitia kwa ufupi historia hiyo ya Mzee Ruksa yaani Ally Hassan Mwinyi Mtandao wa timesmajira na wafanyakazi wote wanamtakia maisha marefu zaidi na kumtaka aendelee kujikinga na ugonjwa hatari wa Corona ambao umekabili Dunia kwa Sasa.