April 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya ardhi ilivyopiga hatua utoaji huduma sekta ya ardhi kwa wananchi

WAKATI Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikikaribia kuwasilisha makadirio yake ya Bajeti 2020/2021, Mei 11,2020 Wizara hiyo imeendelea kupiga hatua katika utekelezaji wa shughuli zake mbalimbali na kuifanya kuwa moja ya Wizara zilizoweza kupunguza na kukidhi kiu ya wananchi katika masuala ya ardhi.

Hali hiyo inafuatia juhudi kubwa zinazofanywa na Mawaziri wenye dhamana pamoja na Watendaji idara mbalimbali zilizopo chini ya Wizara hiyo katika kuhakikisha huduma za sekta ya ardhi zinatolewa kwa ufanisi na kumsaidia mwananchi na wakati huo kuiwezesha serikali kuongeza mapato kupitia kodi ya pango la ardhi.

Katika moja ya hatua kubwa inayoweza kuelezwa kuwa imeweka historia ni uamuzi wa Wizara kusogeza huduma za sekta ya ardhi kwa wananchi kwa kuanzisha ofisi za Ardhi katika mikoa yote ya Tanzania Bara .

Awali huduma za sekta ya ardhi zilikuwa zikitolewa kwenye ofisi za ardhi za Kanda ambapo kanda moja ilikuwa ikihudumia zaidi ya mikoa mitatu.

“Uanzishwaji Ofisi za Ardhi za mikoa siyo tu utawapunguzia usumbufu wa wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za ardhi ofisi za kanda bali utaokoa fedha za serikali hususan katika ofisi zake za ardhi kwenye halmashauri za wilaya ambazo zilikuwa zikiwatuma maafisa wake kupeleka nyaraka za ardhi ofisi za Kanda’’ anasema Waziri wa Ardhi William Lukuvi.

Kwa mfano mwananchi kutoka mkoa wa Katavi ilimlazimu kwenda ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda iliyopo katika mkoa wa Tabora jambo linalomfanya kutumia kiasi kikubwa cha fedha kama nauli na gharama nyingine za malazi tofauti na malipo aliyoyafanya kwa ajili ya kupata hati.

Vile vile, suala hilo limezifanya ofisi za ardhi katika halmashauri mbalimbali kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kuwatuma maofisa wake kupeleka ama kufuatilia nyaraka za ardhi ofisi za Kanda na uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa kutazifanya sasa halmashauri kutoingia tena gharama hizo kwa kuwa huduma zote zitakuwa zinapatikana katika mikoa husika.

Tayari ofisi za ardhi za mikoa zimeanza kufanya kazi kwa kutoa huduma zilizokuwa zikitolewa ofisi za ardhi za Kanda.

Huduma hizo ni pamoja na Upimaji, Upangaji, Uthamini na Usajili Hati ambazo kwa pamoja zinaifanya Wizara kukidhi kiu ya muda mrefu ya wananchi kupata huduma za ardhi karibu na maeneo yao.

Aidha, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika hatua nyingine ya kuhakikisha kumbukumbu zake za ardhi zinatunzwa na kuhifadhiwa katika mazingira salama sambamba na kupata milki yake kwa haraka ilianzisha mfumo unganishi wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi (ILMIS) wenye lengo la kuboresha utunzaji kumbukumbu na nyaraka za ardhi, kurahisisha utendaji kazi, kuharakisha mchakato wa utoaji wa milki.

Uanzishwaji mfumo huo unafanyika kwa awamu na awamu ya kwanza ulihusisha Ukarabati wa jengo la Kituo cha Kutunza Kumbukumbu za Ardhi katika Jiji la Dar es Salaam (National Land Information Centre), Kusimika Mfumo wa ILMIS katika ofisi ya Kanda ya Dar es Salaam na Manispaa za Kinondoni, Ubungo, Kigamboni na Temeke.

Kupitia mfumo huo tayari kumbukumbu za majalada 728,370 ya usajili wa hati, upimaji na umilikishaji wa ardhi yamebadilishwa kutoka analogia kuwa digitali.

Aidha Miamala 254,944 na viwanja 239,317 vimeingizwa kwenye mfumo wa ILMIS ambapo jumla ya Hatimiliki ya ardhi za kielektroniki 3,868 ziliandaliwa na kutolewa kwa njia ya kielektroniki.

Ujenzi wa Mfumo wa ILMIS ulihusisha pia ujenzi wa kituo cha Taifa cha Kumbukumbu za Ardhi ambacho kitatumika kuhifadhi kumbukumbu zote za ardhi kwa njia ya kielektroniki kwa nchi nzima. Mfumo wa aina hii utaenezwa katika mikoa iliyobaki na halmashauri zote nchini.

Sambamba na hatua inazochukua kuboresha utoaji huduma za Ardhi, pia Wizara ya Ardhi imeendelea na juhudi mbalimbali za kuhakikisha migogoro ya ardhi inatatuliwa kwa njia ya amani.

Jitihada hizo ni pamoja na kutatua migogoro ya ardhi kupitia program ya Funguka kwa Waziri pamoja kukamilisha maandalizi ya Mpango Mkakati wa kumaliza migogoro ya matumizi ya ardhi kwa kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini.

Aidha, katika kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi jumla ya vijiji 920 kati ya 975 vilivyokuwemo ndani ya hifadhi na mapori vilivyokuwa na migogoro ya ardhi na maeneo ya hifadhi vimehalalishwa rasmi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii baada ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta wakiongozwa na Waziri wa Ardhi kufanya ukaguzi na kupeleka mapendekezo kwa Rais John Pombe Magufuli aliyeridhia vijiji 920 kubaki katika maeneo ya hifadhi.

Pamoja na hayo, zaidi ya migogoro ya matumizi ya ardhi 10,000 imetatuliwa kiutawala kupitia juhudi za viongozi wa Wizara na watendaji katika ngazi mbalimbali ambapo katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano, jumla ya mashauri 79,753 yameamuliwa kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.

Katika kuchangia ongezeko la mapato ya Serikali, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kukusanya kodi kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Sekta ya Ardhi nchini.

Kiwango cha makusanyo yatokanayo na sekta ya ardhi kimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 54.1 katika mwaka wa fedha 2015/16 hadi wastani wa Bilioni 100 kwa mwaka 2019/20.

‘’Kodi ya Pango la Ardhi siyo tu inaisaidia serikali kuongeza mapato yake bali inaisaidia pia utekelezaji miradi yake ya kimkakati kama vile ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Mradi wa kukufua Umeme wa Mwl Nyerere- Rufiji na miradi mingine’’ anasema Naibu Waziri wa Ardhi Dkt.Angeline Mabula

Ongezeko la makusanyo hayo limetokana na juhudi za Wizara za kudhibiti mifumo ya ukadiriaji kodi ya pango la ardhi, pamoja na kurahisisha njia za ulipaji. Kwa sasa Wizara imerahisha zaidi kujua unadaiwa kiasi gani cha kodi ya pango la ardhi na kulipia kwa kutumia mitandao ya simu za mkononi.

Hizo ni baadhi tu ya juhudi ‘lukuki’ za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha mwananchi anapata huduma za sekta ya ardhi zenye ufanisi na zilizo bora kuanzia upangaji hadi umiliki na hatimaye mwananchi mbali na mambo mengine kuitumia milki yake ya ardhi katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi.