June 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kihongosi:Viongozi msitunishiane misuli

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Manyara.

KATIBU wa NEC,Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kenani Kihongosi, ametoa onyo kwa viongozi wa serikali na Chama wanaotunishiana misuli, huku akikisitiza kuwa atakaye fanya hivyo atashughulikiwa kwenye maamuzi ya vikao.

Alisema lazima kila mmoja aliyepewa dhamana ajue anamuwakilisha Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, hivyo viongozi hao wafanye kazi kwa umoja, ushirikiano na uadilifu mkubwa.

Akizungumza leo Juni 3, 2026 na wanachama wa shina namba nane tawi la Tunduru Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Kihongosi amesema, viongozi wa Chama na serikali wakishirikiana hata fursa zinapokuja watafanya kazi kwa pamoja na wanachi watafurahia maendeleo.

“Hatupaswi kutunishiana misuli au kuvimba kwa vyeo tulivyonavyo tunachohitaji ni kazi kama kuna mtu ana amini tunatania (CCM) afanye mambo yasiyo aone alafu tutakutana kwenye maamuzi ya vikao, lazima kila mmoja aliyepewa dhamana ajue ana muwakilisha Rais.”amesema.

Pia amesisitiza kuwa, CCM hakihitaji kuona vurugu wala makundi katika maeneo yoyote ikiwemo Wilaya hiyo ya Simanjiro.

Aidha Kihongosi amewataka wananchi wa Simanjiro kuhakikisha kipaumbele chao ni usalama wao, huku akiwataka kutokubali kushawishiwa kuharibu miundombinu ya nchi kwa maslahi ya watu binfasi.

Pia amewataka wananchi hao kutokubali kuapandikizwa chuki ya kuvichukia vyombo vya usalama (Jeshi la Polisi) ambapo alidai kuna watu wasiotakia mema amani wanafanya kazi hiyo.

“Tusipandikizwe chuki juu ya vyombo vyetu amani ikitoweka hutafanya jambo lolote lazima tudumishe umoja wa Kitaifa, amani na upendo wa nchi yetu.”amesema Kihongosi.

Aidha Kihongosi ameongeza kuwa CCM itabaki kuwa kimbilio la watu bila kubabua itikadi za dini, ukabila na ukanda katika kuleta maendeleo kwa wananchi.