May 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Safari ya asilimia 100:Hatua kwa hatua kidato cha kwanza walivyoripoti shuleni 

Na Judith Ferdinand

Mwanzoni mwa muhula wa kwanza wa masomo mwaka 2026, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza ilikabiliwa na changamoto ya idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kutoripoti shuleni kwa wakati.

Hadi Februari 5, 2026, wanafunzi 9,897 kati ya 11,348 waliopangiwa kujiunga na kidato cha kwanza walikuwa wameripoti shuleni, sawa na asilimia 87, huku wanafunzi 1,451 sawa na asilimia 13 wakiwa bado hawajafika.

Katika kufahamu zaidi namna gani Halmashauri hiyo itafanikisha wanafunzi  wa kidato cha kwanza waliopangiwa  wanaripoti, Februari 6,2026 ikiwa na asubuhi tulivu,nafunga safari hadi makao makuu ya Halmshauri ya Manispaa ya Ilemela iliopo Buswelu.

Napokelewa kwa bashasha na Ofisa Elimu Maalumu Sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Mwalimu Mugyabuso Witness,na mazungumzo yetu yanaanza,anasema 

kati ya wanafunzi  waliopangiwa kati halmshauri hiyo,wavulana walikuwa 5,474 na wasichana 5,874. Walioripoti hadi  kufikia Februari 5,2026 walikuwa wavulana 4,785 na wasichana 5,112.

Hata hivyo, hali hiyo haikudumu kwa muda mrefu, kwani ilizindua mfululizo wa hatua za kimkakati zilizozaa matokeo chanya.

Hatua ya kwanza: Ufuatiliaji wa takwimu na mahudhurio

Mwl.Mugyabuso anaeleza kuwa,halmashauri ilianza kwa kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa mahudhurio kupitia shule zote za Serikali na binafsi.

Anaeleza kuwa walitegemea taarifa za kila siku kutoka kwa walimu wakuu kubaini wanafunzi ambao hawajaripoti.

“Mwanafunzi anapokosa kufika shuleni kwa siku kadhaa, mzazi au mlezi huitwa katika ngazi ya kata kwa hatua zaidi za ufuatiliaji na kisheria,” anasema.

Hatua ya pili: Ushirikishwaji wa jamii

Mwl.Mugyabuso,anasema Katika kuongeza nguvu ya ufuatiliaji, halmashauri iliwahusisha viongozi wa mitaa, watendaji wa kata na jamii kwa ujumla.

Pia waliwatumia wanafunzi waliokwisha ripoti shuleni  kama mabalozi wa elimu kwa kuwatafuta wenzao katika maeneo yao na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.

“Tunatumia hata wanafunzi waliopo shuleni kuulizia wenzao mitaani. Wakibaini mwanafunzi amehamia shule binafsi bila taarifa, tunafuatilia,” anaeleza Mwl.Mugyabuso.

Hatua ya tatu: Kushughulikia changamoto za taarifa na uhamisho

Mwl.Mugyabuso,anasema miongoni mwa changamoto zilizobainika katika kipindi hicho  ni baadhi ya wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi bila kutoa taarifa rasmi kwa shule walizopangiwa.

“Wazazi wengi hutoa taarifa wanapohitaji namba ya PREM, na wakati huo tayari muda wa kuripoti unakuwa umepita,” anabainisha  Mwl.Mugyabuso.

Hatua ya nne: Kuondoa vikwazo vya mahitaji ya shule

Anasema,halmashauri pia ilichukua hatua ya kuruhusu wanafunzi kuanza masomo hata kama hawajakamilisha mahitaji muhimu kama sare, viatu na madaftari,ili kuondoa kikwazo kwa wazazi wenye uwezo mdogo wa kifedha.

“Serikali inatoa elimu bila malipo, hivyo hakuna mtoto anayepaswa kukosa shule kwa kukosa mahitaji.Waliruhusiwa kuanza huku wazazi wakiendelea kujipanga,” anasisitiza Mwl. Mugyabuso.

Hatua ya tano: Uhamasishaji wa kijamii na mikutano ya hadhara

Katika ngazi ya jamii, viongozi waliendesha mikutano ya hadhara kuhamasisha wazazi na walezi,ambapo Diwani wa Kata ya Kayenze, James Makambuya, anasema walikumbana na changamoto ya mtazamo hasi kwa baadhi ya wazazi.

“Kuna wazazi wanaamini elimu haina manufaa kwa kuwa ajira ni chache. Tulilazimika kubadilisha mtazamo huo. Mazingira ya kiuchumi na shughuli za uvuvi yalichangia baadhi ya wanafunzi kuchelewa kuripoti,”anasema Makambuya.

Hatua ya sita: Tofauti ya mwitikio kati ya shule

Katika kipindi hicho, baadhi ya shule zilikuwa na mwitikio mdogo, ikiwemo Nyasaka asilimia 62, Shibula asilimia 68, Lubuka asilimia 51 na Angeline Mabula asilimia 66.

Kwa upande mwingine, shule kama Lumala, Nundu, Nyamanoro na Pasiansi zilifikia asilimia 100 mapema, huku Ibungiro ikifikia asilimia 99.9.

Hatua ya saba: Maboresho ya mazingira ya kujifunzia

Shule ziliendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kupokea wanafunzi,ambapo shule ya sekondari Bujingwa, Mkuu wa shule hiyo, Magweiga Magabe, anasema kati ya wanafunzi 538 waliopangiwa, asilimia 99.44 walikuwa wameripoti, wakiwemo waliobaki shuleni na waliokwenda shule binafsi hadi kufikia Februari 5,2026.

Anaeleza kuwa changamoto  kwa wanafunzi wapya ni lugha ya kiingereza, hivyo shule ilianzisha mafunzo  ya  wiki sita ya awali.

“Wanafunzi wengi wanatoka katika mazingira ya kutumia kiswahili, hivyo wanapata changamoto wanapoanza kutumia kiingereza katika masomo,” anasema.

Aidha, anasema shule hiyo ina miundombinu ya kutosha na imepokea shilingi milioni 25 kwa ajili ya ujenzi wa  madarasa mawili.

Hatua ya nane: Mtazamo wa wanafunzi

Baadhi ya wanafunzi wameeleza namna wanavyojipanga kukabiliana na changamoto hizo.

Careen Philipo anasema ni muhimu kuimarisha ufundishaji wa kiingereza kuanzia shule za msingi, huku Eunice Miguel akisisitiza umuhimu wa vitabu na vifaa vya kujifunzia huku akiwahimiza wanafunzi wa kike kujikita katika masomo ya sayansi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Hatua ya tisa: Mafanikio ya hatua kwa hatua

Juhudi hizo zilianza kuonesha matokeo, ambapo hadi Februari 19, 2026, wanafunzi 10,994 sawa na asilimia 97 walikuwa wameripoti.

Mwl.Mugyabuso anaeleza kuwa walikuwa na matumaini ya kufikia asilimia 100 kabla ya mwisho wa Februari.

Hatua ya mwisho: Mafanikio kamili

Aprili 24,2026,majira ilibisha hodi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa lengo la kufahamu idadi ya kidato cha kwanza mwaka huu walioripoti baada ya zoezi kuhitimishwa Machi 31,2026.

Na mazungumzo yetu na Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Mwl. Sylvester Mlimi,yanaanza kwa kusema,hadi kufikia Machi 31, 2026, wanafunzi wote 11,348 wa kidato cha kwanza walikuwa wameripoti shuleni, sawa na asilimia 100.

Mwl.Mlimi,nasema mafanikio hayo yalitokana na maandalizi ya mapema yaliyoanza Desemba 2025, ikiwa ni pamoja na uundaji wa timu za mapokezi na uhamasishaji kupitia vyombo mbalimbali.Pia halmashauri iliweka utaratibu wa kupokea taarifa za mahudhurio kila siku ya wanafunzi.kwa kila shule hatua iliyosaidia halmashauri kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa msukumo pale ilipobidi.

Pia anasema waliruhusu wanafunzi kuanza masomo hata kama hawajakamilisha sare pamoja na kuwasaidia wazazi ambao watoto wao walipangiwa shule za mbali kubadili pale ilipohitajika.

“Kwa kufanya hivyo tumefanikiwa kabla ya Machi 31,2026, watoto wote asilimia 100 wa kidato cha kwanza walikuwa wameisha ripoti shuleni na wapo wanaendelea na masomo yao kama kawaida,”anasema Mwl. Mlimi na kuongeza:

“Mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa wazazi na wadau huku halmashauri ikiwa na shule 35 ambapo 34 zinapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza,uwezo wa shule hizo upo vizuri ndio maana wanafunzi wote wamepokelewa kama ilivyopangwa, miundombinuna mazingira ya kusoma ni mazuri na walimu wapo kwa kila shule,”.

Mkakati wa Halmashauri 

Mwl.Mlimi, anasema halmashauri imeendelea kuimarisha mazingira ya elimu, ikiwa ni pamoja na utoaji wa chakula shuleni, michezo na uwepo wa walimu wa kutosha na  imejipanga kuhakikisha wanafunzi hao wa kidato cha kwanza wanamaliza elimu yao ya sekondari kwa kila shule inakuwa na walimu mahiri kwa ajili ya kuwafundisha.

“Watoto hao ni wadogo,wamezoea kuishi mazingira ya shule ya msingi ambao wanatumia lugha ya  Kiswahili.  Tunahakikisha tunapanga walimu wenye weledi ambao watawalea,kuwasikiliza na kuwavumilia,lengo ni kuwapa motisha wanafunzi hao waone suala la kujifunza kwao ni la msingi,”.

Sanjari na hayo,wanakuwa na vikao vya wazazi ambavyo wanavisimamia kwa kila shule,ili kuwafahamisha kuwa suala la mtoto kuendelea na masomo ni la kisheria na kiuratibu siyo hiari.Mtoto kwenda shule,maana yake ni fursa na haki yake,hivyo aliwaomba wazazi watoe ushirikiano kwa kuwahimiza watoto wao kwenda shule Kwa wakati.

“Kwa mzazi ambaye hanaelekea kutuangusha au kutukwamisha, tunachukua hatua kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya.Serikali imeandaa miundombinu mizuri ya shule na kuajiri walimu hivyo,hatuna sababu ya kukwamisha wanafunzi kwenda shule,”.

Kwa ujumla, safari ya Ilemela inaonesha kuwa kupitia ufuatiliaji, ushirikiano wa jamii na sera rafiki za elimu, inawezekana kufikia lengo la kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya elimu.