NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Denis Londo, ametembelea banda la Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) katika Maonesho ya Kimataifa ya Mbeya City Expo 2026 yanayoendelea katika viwanja vya Uhindini, jijini Mbeya, ambapo alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi hiyo katika kulinda maslahi ya walaji na kuimarisha ushindani wa biashara nchini.
Katika maonesho hayo, FCC imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kuhusu haki za mlaji, namna ya kutambua na kuepuka bidhaa bandia pamoja na umuhimu wa ushindani wa haki katika shughuli za biashara.
Elimu hiyo imevutia mamia ya wananchi waliojitokeza kutembelea banda hilo na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu biashara, ushindani na ulinzi wa walaji.
Akizungumza wakati akifunga Maonesho hayo yaliyodumu kwa siku tisa Mei 30, 2026 jijini Mbeya, Naibu Waziri Londo alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya bidhaa bandia, akieleza kuwa bidhaa hizo zinaathiri afya za watumiaji, kudhoofisha biashara halali na kupunguza mapato ya Serikali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kanda wa FCC – Nyanda za Juu Kusini Bw. Dickson Mbanga, amesema taasisi hiyo imejipanga kuendelea kuimarisha kampeni za utoaji elimu kwa wananchi ili kuwajengea uwezo wa kutambua bidhaa halisi na kuepuka kununua au kutumia bidhaa zisizo na viwango vinavyotakiwa.
Mbanga alisema Maonesho ya Mbeya City Expo yamekuwa jukwaa muhimu la kuifikia jamii kwa karibu na kutoa elimu inayolenga kuongeza uelewa kuhusu sheria za ushindani na hatua zinazochukuliwa dhidi ya wafanyabiashara wanaojihusisha na usambazaji wa bidhaa bandia.
“Tunatumia maonesho haya kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwaelimisha kuhusu hatari za bidhaa bandia na kumlinda mlaji. Lengo letu ni kuhakikisha watumiaji wanakuwa na taarifa sahihi zitakazowasaidia kufanya maamuzi bora wanaponunua bidhaa mbalimbali sokoni,” alisema Mbanga.
Aliongeza kuwa FCC itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa biashara na vyombo vya usalama katika kudhibiti bidhaa bandia zinazoingia sokoni, huku ikiendelea kuhamasisha wananchi kutoa taarifa wanapobaini uwepo wa bidhaa zinazotiliwa shaka.
Maonesho ya Mbeya City Expo 2026 yamewakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali za uchumi, biashara na uwekezaji, huku yakitoa fursa kwa taasisi za umma na binafsi kuonesha huduma, bidhaa na mafanikio yao kwa wananchi. Kupitia ushiriki wake, FCC imeendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya kulinda walaji na kujenga mazingira ya biashara yenye ushindani wa haki.

More Stories
TASAC ,NBS zashirikiana sensa vyombo Majini
Kihongosi:Viongozi msitunishiane misuli
Airtel, ZECO zaingia ushirikiano kuimarisha Huduma za Kidigitali