April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vinyago vinavyochongwa na baadhi ya vijana nchini ili kujipatia kipato

Vijana kupatiwa elimu ya kujitambua, kujiletea maendeleo

Na Mwandishi Wetu, timesmajira online, Dodoma .

KIKUNDI cha Umoja wa Vijana, Jijini Dodoma (Protect Me Movement), kimepanga kuwa na kampeni maalum ya kuwaongezea uelewa mzuri wa maendeleo ili waweze kujitambua na kupambana na changamoto wanazokutana nazo pindi wanapokuwa shuleni na vyuoni.

Hatua hiyo itawawezesha kujiajiri wenyewe pindi wanapokuwa hawana ajira rasmi.

Hayo yamesema Jijini Dodoma jana na mhasisi wa kikundi hicho, Erick Msemwa, alipokuwa akieleza namna ya vijana waliopata elimu, wanavyoweza kuitumia hata pale wanapokosa ajira.

“Sisi ni umoja wa vijana tuliojitolea kuwasaidia vijana wenzetu katika masuala ya kujitambua ili kuwawezesha kupambana na kukabiliana na changamoto za kijamii na za kiuchumi,”amesema Msemwa.

Aidha, Msemwa amesema elimu hiyo itawapatia taarifa sahihi na maarifa yatakayowawezesha vijana kutimiza malengo na ndoto zao.

Pia amesema wamedhamiria kuisaidia Serikali kwa kuwaelimisha vijana ili kupunguza tabia hatarishi. Alizitaja baadhi ya tabia hatarishi ambazo zinatokanazo na ukosefu wa kutojitambua kwa vijana wengi kama vile matumizi ya dawa za kulevya, pombe na kutumia vibaya mitandao ya kijamii.

Ameongeza kuwa nia ya kikundi hicho hicho ni kuona vijana wanabadilika na kubadili mitazamo hasi ili wawe chachu ya maendeleo ya jamii kwa kuwaongezea elimu na ujuzi wa kujitambua.

Kwa uponde mwingine ameiomba Serikali iwaunge mkono kwa kuwakutanisha na wadau ambao watashirikiana nao kwa kuwawezesha, ili waweze kuifikia jamii, hasa vijana kwani ndilo kundi kubwa na linalohitaji msaada zaidi ili kuiletea maendeleo Tanzania.