April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Daniel Mtuka, akimnadi mgombea wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Dkt.Pius Chaya wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Manyoni Mashariki.

Dkt. Chanya ataja vipaumbele akichaguliwa Manyoni Mashariki

Na Joyce Kasiki, timesmajira, Online Manyoni

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Pius Chaya, ametaja vipaumbele sita atakavyovishughulikia katika kipindi chake cha uongozi akipata ridhaa kutoka kwa wananchi wa jimbo hilo.

Ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na afya, maji, elimu, kilimo, michezo na ajira.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi katika jimbo hilo wilayani Manyoni mkoani Singida, Dkt.Chaya amesema utekelezaji wa vipaumbele hivyo utasaidia kuondoa changamoto kadhaa zilizopo jimboni humo.

Kuhusu afya, amesema katika kipindi chake wake atahakikisha anapigania upatikanaji wa hospitali ya wilaya ili kurahisisha huduma za matibabu hasa kwa wajawazito na watoto.

Amesema atahakikisha akina mama wajawazito wanaosubiri kujifungua wanakuwa na jengo la kisasa badala ya jengo wanalotumia hivi sasa, ambalo alidai halina hadhi.

“Sasa hivi akina mama wajawazito wanaotoka vijijini na kusubiria kujifungua wanakaa jengo la tumbaku,hii siyo sawa nitapigania upatikanaji wa jengo la kisasa kwa ajili ya akina mama hawa.” amesema.

Kuhusu maji, amesema atahakikisha ndani ya mwaka mmoja tatizo la maji katika jimbo hilo litabaki historia. Dkt.Chaya amezungunzia kuhusu elimu ambapo amesema, liicha ya Serikali kufanya mambo mengi katika sekta ya hiyo lakini bado kuna changamoto katika eneo hilo, huku akisema kuna baadhi ya kata hazina shule za sekondari lakini pia zipo shule za msingi ambazo hazijasajili.

“Nikipata ubunge nitahakikisha nasimamia usajili wa shule zote ambazo hazijasajiliwa, lakini pia kuwa na sekondari katika kata, haya yote yatasaidia watoto kutotembea umbali mrefu kwenda shuleni,” amesema Dkt.Chaya na kuongeza kuwa

“Pia nitaweka vipaumbele kwenye ujenzi wa hosteli kwa ajili ya kuwalibda watoto wa kike na nitashughulikia upatikanaji wa madawati mashuleni.”

Kuhusu masuala ya ajira, amesema atalishughulikia suala hilo hususan katika kuwajengea uwezo wasomi na wasio wasomi ili waweze kuajirika na kujiajiriwa.