April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waendesha bodaboda wakisubiri wateja

Profesa Kitila kurasimisha shughuli za waendasha bodaboda, bajaj Ubungo

Na Mwandishi Wetu, timesmajira, online Dar

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Ubungo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Profesa Kitila Mkumbo, amewahakikishia wana-Ubungo wa vyama vyote kuwa endapo watampa ridhaa ya uwakilishi atashughulikia kero za maji, miundombinu ya barabara za mitaa, uboreshaji wa mifumo ya uendeshaji wa masoko, sambambana kurasimisha shughuli za waendesha bodaboda na bajaj na kuwa kazi rasmi tofauti na ilivyo sasa.

Aidha, amesema kadri atakavyojaliwa na Mwenyezi Mungu atahakikisha anachagiza ustawi wa kiwanda cha nguo cha Urafiki ambacho kwa sasa kinaendeshwa kwa kusuasua ili kiwe mhimili wa ajira kwa vijana na ustawi wa maendeleo kwa tija ya wana-ubungo wote na taifa kwa ujumla.

Profesa Mkumbo ameyasema hayo juzi wakati akinadi sera, ilani ya CCM na shabaha ya shughuli zake za kibunge kwa wakazi wa Shirika la Nyumba na maeneo ya Urafiki, Kata ya Ubungo, kwenye viwanja vya Kinesi jijini Dar es Salaam.

“Kiwanda chetu cha Urafiki mpaka sasa kinaendeshwa kwa kusuasua na wasihi ni kiwaomba mnipe ridhaa ili niwe sehemu kubwa ya ushawishi wa kuleta ustawi mpya wa kiwanda cha Urafiki ambacho kwa sasa kinaendeshwa kwa kusuasua ili kiwe mhimili wa ajira kwa vijana na ustawi wa maendeleo kwa tija kwa wana ubungo wote na taifa kwa ujumla ,” alisema Mkumbo

Akifafanua dhana ya kurasimisha ajira za vijana takribani elfu tatu waliojiajiri kuendesha bodaboda na bajaj waliopo ndani ya jimbo la Ubungo, Profesa Mkumbo alisema atahakikisha kazi hiyo inarasimishwa na kuwa ajira rasmi.

Waendesha bajaj wakisubiri wateja

“Haiwezekani nasio sawa hata kidogo bodaboda na bajaj akikamatwa na askari hapewi ‘notifications’ yoyote anawekwandani na chombo chake pia kinazuiliwa…sio sawa,” alisema Profesa Mkumbo na kuhoji;

“Mbona madereva wa magari wanapewa muda wa hadi siku saba kulipa faini?”.

Akizungumzia kero za ubovu wa miundombinu ya barabara za mitaa alisema endapo wana-ubungo watampa ridhaa atahakikisha anashawishi kufanyika maboresho na matengenezo yauhakika ya barabara zote korofi ndani ya jimbo hilo kwa kujenga hoja kwenye Baraza la Halmashauri kuanza kutenga walau asilimia 3 mpaka 5 ya mapato yake ili kushughulikia kero hiyo.