May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaridhishwa mapinduzi viwanda vya dawa, vifaa tiba

Na Mwandishi Wetu, TimesMajiraOnline, Njombe

SERIKALI imeridhishwa na mapinduzi yaliyofanyika katika sekta ya viwanda hususani upande wa viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini.

Hatua hiyo inatokana na Rais Dk. Samia kuelendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya viwanda na miradi yote ya maendeleo iliyoanzishwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Hayo yamesemwa juzi mkoani Njombe na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati wa ukaguzi wa uzalishaji wa kiwanda cha mipira ya mikono (gloves) kilichopo Idofi Mkoani Njombe kinachosimamiwa na Bohari ya Dawa (MSD).

Kiwanda hicho kinatarajiwa kuwekwa jiwe la misingi na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, kesho.

Amesema ujenzi na uzalishaji wa kiwanda cha mipira ya mikono Idofi kinachosimamiwa na MSD unaridhisha na kukidhi mahitaji.

Amefafanua kuwa uwekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba unaofanywa na Serikali unaenda kupunguza uagizaji wa bidhaa nje ya nchi na matumizi ya fedha za kigeni.

Ameeleza kuwa, katika hatua ya uwekezaji wa kiwanda hicho, Rais Samia alikuta ujenzi wake ukiwa asilimia 30 na sasa ni asilimia 90.

“Lengo la Serikali ya Rais Dtk. Samia ni kufikia asilimia 50 kutoka asilimia 15 iliyopo sasa katika ununuzi wa bidhaa za afya ndani ya nchi kufikia mwaka 2030,”alisema.

Amesema kwasasa vifaa vya afya kwa asilimia 85 vinanunuliwa kutoka nje na hiyo ina changamoto zake ikiwemo kusubiri kwa miezi tisa bidhaa kufika, hali inayosababisha uhaba wa dawa na kuongezeka matumizi ya fedha za kigeni.

Waziri Ummy amesisitiza kwa sasa kuna viwanda 30 vya dawa na vifaa tiba vya ndani na kati ya hivyo 11 vinafanya kazi.

Ameongeza kwamba tayari serikali imetoa zaidi ya sh. Bilioni 11 ya uendelezaji wa kiwanda hicho na kudhamiria kuongeza uzalishaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba.

“Nipongeze sana Bodi ya MSD hapa tunazungumzia bidhaa za afya za watu, lazima kujiridhidhisha wamefanya hivyo na kiwanda kiko vizuri ambapo tutakifungua kabla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa,”alifafanua.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, amesema kiwanda hicho kimeanza uzalishaji wa awali na kinatararajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Amesema kiwanda hicho hadi kukamilike kitagharimu sh. bilioni 22.5.

Amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi na ufungaji wa mitambo, kiwanda hiki kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mipira ya mikono 20,000 kwa saa sawa na jozi (pairs) 10,000 na hivyo kufanya uzalishaji wa takribani jozi 86,400,000 kwa mwaka.

“Hii ni sawa na asilimia 83.4 ya makadirio ya mahitaji ya mipira ya mikono nchini ya jozi milioni 104 kwa mujibu maoteo ya uhitaji ya bidhaa za gloves nchini kwa mwaka 2023/2024,”alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka amesema, Rais Dkt. Samia amefanya mabadiliko makubwa katika kiwanda hicho na amedhamiria kuona uzalishaji wake unakuwa na tija kwa Watanzania na hasa wananchi wa Njombe ambao wameanza kunufaika na fursa zilizopo hususani kupata kipaumbele katika ajira.