April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uchimbaji wa makaa ya mawe mkoa wa Songwe kuongeza pato la Taifa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

KIASI cha  Shilingi bilioni 250 zinatarajiwa kuzalishwa katika kipindi cha miaka mitano  kupitia mkataba wa mauziano wa tani 60,000 kwa kampuni ya Kimataifa ya uchimbaji Makaa ya Mawe nchini Uswis  (ABSA).

Akizungumza jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini mkataba wa Makaa ya Mawe ya Mkoa ya Songwe katika Mgodi wa Kabulo kupitia kampuni ya ABSA, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt.Venance Mwasse amesema,mkataba huo unakwenda kuongeza mapato zaidi.

“Kwa hiyo  mkataba huu ni mkubwa na  ni wa kihistoria  kwa nchi kwa kuwa utasaida kwenye masuala ya kiuchumi.”amesema na kuongeza kuwa

“Makaa hayo yatasafirishwa kutoka Kiwira hadi Bandari ya Mtwara na tayari magari 300 yatakayokuwa na madereva wawili kila moja yameandaliwa hivyo watakuwa 600 jumla, pia kutakuwa na nguvu kazi takribani watu 200,”

Dkt.Mwasse amesema,mkataba huo utatekelezwa  kupitia vifungu walivyokubaliana na mwekezaji huyo huku akimuhakikishia kuwa yupo  kwenye mikono salama na  matokeo mazuri na huduma wataziona wakati wa utekelezaji wa mradi wa uchimbaji makaa hayo ya mawe.

Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa amesema Serikali kupitia shirika la STAMICO itakusanya mapato wastani wa shilingi bilioni 4.16 kwa mwezi sawa na wastani wa shilingi bilioni 50 kwa mwaka.

Mbali hilo pia Shirika litatoa  ajira kwa vijana wa kitanzania zisizo za moja kwa moja 600 na fursa nyingine kupitia mradi huo.

“Ni matumaini yangu makubaliano tuliyokubaliana ABSA yataleta tija katika nchi hizo na kuishukuru STAMICO kwa maamuzi ya kukubaliana kufanya biashara nchini ambapo itasaidia kuwapatia vijana ajira.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Kampuni ya ABSA, Gerges Schmickrath ameishukuru wizara ya Nishati kupitiaShirika lake la STAMICO kwa kuiamini kampuni yake na hatimaye kupata kibali cha kuwekeza  katika mradi wa makaa ya mawe ambao amesema utakuwa na manufaa kwa watanzania na Taifa kwa ujumla.

Schmickrath amesema kutokana na Serikali kuonyesha imani kwao na wao watafanya kazi itakayoleta tija kama ilivyokusudiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Drumlin Construction LTD ambaye ni msafirishaji wa makaa hayo nchini, Linus Seushy amesema kuwa wamejiandaa kuhakikisha kila kitu kinafanyika kama kilivyopangwa kwa maslahi mapana kwa Taifa.