April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania kunufaika na elimu kuhusu sekta ya mafuta na gesi asilia

 Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

 MAMLAKA  ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema kuwa imejipanga kutoa elimu kwa watanzania   juu ya  sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia  kwenye Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi mkoani Morogoro.

Wataalamu kutoka PURA  wamejipanga kukuza uelewa wa sekta hiyo ili kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye sekta husika.

 Maonesho hayo yamefunguliwa juzi  na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigela katika viwanja vya Jamhuri mkoani humo na kuendelea hadi Mei 14, 2022 ambapo yanatarajiwa kuhitimishwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Baadhi ya masuala yatakayozungumziwa kwenye banda la PURA  katika maonesho ni pamoja na mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi asilia, mnyororo wa thamani wa mradi wa kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia zinazoendelea nchini.

Maeneo mengine ni ushiriki wa wazawa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mkondo wa juu wa petroli na fursa zinazopatikana kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo,  Shigela amesema maonesho hayo ni fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kazi na washiriki wengine kuhusu fursa mbalimbali na changamoto zinazowakabili na jinsi ya kukabiliana nazo.

“Maonesho haya ni ya muhimu kwani yanatoa elimu kwa wananchi ambayo inawawezesha kushiriki kwa wingi na kwa ubora kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo,” amesema.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’i Issa amesema maonesho hayo kwa mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “uchumi imara kwa maendeleo endelevu”.

Ameongeza kuwa lengo la maonesho hayo ni kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu uwepo wa mifuko na programu za uwezeshaji, jinsi ya kujiwekea akiba na jinsia ya kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo.

“Maonesho haya pia yanalenga kutengeneza mtandao wa wafanyabiashara watakaoshiriki na kukuza masoko ya wajasiriali ili kujiletea maendeleo,” amebainisha.