April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPA yatekeleza maelekezo ya Samia kwa kiasi kikubwa

Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline, Dar

MAMAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imefanikiwa kutekeleza kwa mafanikio makubwa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha inakuwa na mifumo Madhubuti ya Tehama.

Kwa mujibu wa taarifa ya TPA, katika mwaka wa fedha 2022/2023 TPA imefanikiwa kukamilika kwa asilimia kubwa mradi wa TEHAMA (Enterprise Resource Planning, ERP) ambao hutumika katika kuandaa na kuhifadhi taarifa za kifedha na kuunganisha shughuli za idara mbalimbali katika kutekeleza majukumu ya kila siku.

“Mfumo huo unaunganisha Idara zote muhimu kwa mfano Idara ya Fedha, Idara ya Rasilimali watu, Idara ya manunuzi na nyinginezo.”

Pia matokeo ya kukamilika kwa mfumo huo, ni sambamba na ufanisi katika uandaaji na utoaji wa taarifa za hesabu za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, ambapo mfumo huo umeiwezesha TPA kupata hati safi kwa miaka miwili mfululizo kwa kaguzi zinazofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

Aidha, kutokana na matumizi ya mfumo huo, TPA imeweza kupata tuzo ya uandaaji bora wa taarifa za hesabu kutoka kwa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).

Zaidi ya hayo, mfumo huo umeongeza tija pia katika kuhakikisha udhibiti wa mianya ya upotevu wa fedha, uandaaji wa taarifa mbalimbali kwa wakati, utunzaji wa nyaraka na taarifa za kifedha na rasilimali za taasisi.

“Kutokana na kuimarika mifumo ya ukusanyaji mapato imepelekea mapato ya TPA kuongezeka kwa asilimia 27 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2021/2022.”

Mafanikio mengine ni kwa upande wa kuhudumia shehena, ambapo kumekua na ongezeko kubwa kwa upande wa meli na shehena ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 idadi ya meli zilizohudumiwa na Bandari za TPA ziliongezeka na kufikia meli 4,762 kutoka meli 4,160 ambazo ni wastani wa ongezeko la asilimia 13.9 kwa mwaka.

Kwa upande wa shehena kiwango cha shehena kilichohudumiwa ni tani milioni 27.8 sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 21.7 ya shehena iliyohudumiwa katika mwaka husika ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Kwa upande wa miundombinu, Mamlaka ya bandari imefanya uboreshaji mkubwa wa miundombinu ikiwemo uundwaji wa mifumo ya TEHAMA, Utekelezaji wa Mradi wa Kimkakati wa Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam (DMGP), Uboreshaji wa Bandari Tanga, Upanuzi wa Bandari ya Mtwara, Uboreshaji wa Bandari za Maziwa Makuu

Uwekezaji huo mkubwa na ununuzi wa mitambo pamoja na ujuzi kwa wafanyakazi umeongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa Mamlaka ya Bandari.