August 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya 186 Wanufaika huduma kupunguza uzito Mloganzila


Na Mwandishi wetu

ZAIDI ya watu 186 wamenufaika na huduma ya kupunguza uzito kwa njia ya puto (Intragastric Balloon) inayotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili–Mloganzila tangu huduma hiyo ilipoanzishwa mwezi Novemba 2022.


Akizungumza kuhusu huduma hiyo, Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Eric Muhumba, amesema huduma hiyo imekuwa suluhisho salama na lenye matokeo chanya kwa watu wenye changamoto ya uzito uliopitiliza.


Amesema hospitali imeendelea kuboresha huduma hiyo kwa kutumia teknolojia za kisasa pamoja na kuwashirikisha wataalamu wa lishe na mazoezi ya mwili ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma jumuishi zinazowasaidia kufikia na kudumisha uzito unaofaa kwa afya bora.


Dkt. Muhumba amesema ubora wa huduma hiyo umeifanya kuvutia wagonjwa kutoka ndani na nje ya Tanzania. Alitaja baadhi ya nchi ambazo wagonjwa wake wametoka kuwa ni Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Malawi.


Aidha, amesema hospitali ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha huduma mpya za kupunguza uzito kwa kutumia sindano na vidonge, hatua inayotarajiwa kuongeza chaguo la matibabu kwa watu wenye changamoto ya uzito uliopitiliza.


Mbali na huduma ya kupunguza uzito kwa njia ya puto, Hospitali ya Taifa Muhimbili–Mloganzila inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kibingwa na ubobezi katika upasuaji, zikiwemo upasuaji wa matundu madogo, upasuaji wa saratani za koo, saratani za kongosho pamoja na upasuaji rekebishi.