Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Mwanza
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limeanza kuchukua hatua na kufanyia kazi malalamiko ya wananchi jijini Mwanza kuhusu mienendo isiyofaa miongoni mwa waendesha pikipiki wasiozingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP.Wilbrod Mutafungwa,akitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari mkoani humo Septemba 16,2026 amesema,malalamiko ambayo jeshi hilo imekuwa ikiyapokea ni pamoja na tabia za madereva hao kuendesha pikipiki kwa mwendo kasi na wa hatari na kusababisha ajali kwao wenyewe pamoja na kuleta hofu kwa watumiaji wengine wa barabara kuhusu usalama wao.

Amesema,madereva hao pia wameongeza na kufunga taa zenye mwanga mkali ambazo siyo rasmi na zinaweza kusababisha ajali kwao na kwa madereva wenzao pamoja na kubadilisha mfumo wa muungurumo wa pikipiki yenye sauti ya juu kuliko kawaida, hivyo kuleta usumbufu kwa wananchi wanaotumia barabara na walio katika shughuli zao.
Pia DCP.Mutafungwa amesema,wamebainisha kuwa wanaendesha pikipiki bila kuwa na namba za usajili, hivyo kuleta wasiwasi na mashaka katika suala la usalama ambapo alisisitiza kuwa vitendo hivyo ni makosa kinyume cha sheria,kanuni na taratibu za usalama barabarani Sura ya 168 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023, kifungu namba 13.
Aidha ameeleza kuwa msako endelevu umeanza Septemba 14 2026 ili kukomesha tabia hizo, na kwamba katika operesheni hiyo wamekamata jumla ya pikipiki 103 na watuhumiwa 30.
Kati ya pikipiki hizo,70 zimekamatwa kwa kosa la kuweka mwanga mkali,13 kwa kosa la kubadili muungurumo, 10 kwa kuendeshwa bila kuwa na namba za usajili, 5 kwa kosa la kutokuwa na leseni na pikipiki 5 zimekamatwa kwa makosa ya kutovaa kofia ngumu (helmet) na kupakizana mishikaki.
Sanjari na hayo Mutafungwa amemuagiza Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza Ibrahim Sunday, kuhakikisha madereva wote waaliokamatwa wanapatiwa elimu na kuziondoa taa zote kwenye pikipiki ambazo haziruhusiwi kisheria pamoja na kuwatoza faini wale wote waliobadili miungurumo ya pikipiki.


More Stories
Mixx, ZANGOF kuziwezesha Asasi za kiraia Zanzibar
Wananchi Ilala wanaoishi mabondeni watakiwa kuhama
Mzizima Derby, vita ya alama, heshima na ubabe leo