Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Dar
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka wananchi wilayani humo mkoani Dar-es-Salaam wanaoishi maeneo hatarishi hususani mabondeni na kwenye mikondo ya maji, kuhama mara moja na kutafuta maeneo salama ili kuepusha maafa yanayoweza kusababishwa na mvua za El-nino zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni.
Ambapo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) imeendelea kutoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mvua za El-nino kuanzia Oktoba 2026.
Mpogolo ametoa agizo hilo Septemba 16,2026 wakati wa ziara yake katika eneo la Viwege, ambapo alizungumza na wananchi wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuwaeleza umuhimu wa kuchukua tahadhari mapema, hasa katika kipindi hiki ambacho mvua kubwa za El-nino zinatarajiwa kuanza.
“Mnafahamu kabisa kuwa maeneo haya mliopo hayaruhusiwi kuishi.Sasa ni vizuri katika kipindi hiki ambacho mvua hazijaanza mtafute mahali salama ili kuepusha maafa yanayoweza kutokea mvua zikianza,”amesema Mpogolo.
Pia amemuelekeza Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini(TARURA) Wilaya ya Ilala kuhakikisha mitaro na mabonde yanasafishwa ili kurahisisha upitishaji wa maji na kupunguza hatari ya mafuriko.
Sanjari na hayo amesema wananchi wanatakiwa kuzingatia maelekezo ya Serikali, kushirikiana na mamlaka husika na kuhakikisha wanachukua hatua mapema kwa ajili ya usalama wao, familia zao na mali zao.
Katika ziara hiyo Mpogolo aliambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar-es-Salaam, Elihuruma Mabelya pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala,Charangwa Selemani,ambapo walitembelea maeneo ya Viwege na Mbondole, Kata ya Majohe, kwa lengo la kutathmini hali ya mazingira na kuchukua hatua za kuimarisha usalama wa wananchi.

More Stories
Mixx, ZANGOF kuziwezesha Asasi za kiraia Zanzibar
Polisi Mwanza yafanyia kazi malalamiko ya wananchi
Mzizima Derby, vita ya alama, heshima na ubabe leo