Na Mwandishi Wetu
MATAJIRI wa Jiji, Azam , leo wanatarajia kuwakaribisha Simba katika pambano la Mzizima Derby, mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na kila upande kuwa na sababu ya kutaka kuibuka na ushindi.
Mchezo huo utakaochezwa saa 1:00 usiku, unatarajiwa kuwa vita kali ya kusaka alama, heshima na ubabe wa soka la Tanzania,
huku Azam ikilinda rekodi yake na Simba ikitaka kuendeleza mwendo wake wa ushindi.
Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na ari kubwa baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, ikifuzu hatua iliyofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-1 dhidi ya Mighty Wanderers.
Katika mafanikio hayo, Clatous Chama ameonekana kurejesha makali yake, akifunga na kusaidia kutengeneza mabao, jambo linaloongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya Simba kuelekea dabi hiyo.
Kwa upande wa Azam, wenyeji wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na jukumu la kulinda rekodi yao ya kutopoteza katika michezo sita ya mwanzo ya ligi, huku wakishinda minne na kutoka sare miwili.
Azam pia inapata nguvu kutokana na kurejea kwa kiungo wake Feisal Salum ‘Fei Toto’, ambaye anatarajiwa kuongeza ubora kwenye eneo la kiungo na kusaidia timu hiyo kukabiliana na presha ya Simba.

Tofauti ya rekodi hizo ndiyo inayoongeza mvutano kwenye mchezo huo, kwani Simba imeanza ligi kwa kushinda michezo yote mitano iliyocheza, wakati Azam ikiwa haijapoteza katika michezo yake sita.


More Stories
Mradi wa Umeme Simiyu wafungua fursa, wachochea Uchumi
FCC yapongezwa kulinda walaji, kuchochea biashara
Waongezewa nguvu huduma za mama wajawazito Same