Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza
WAJASIRIAMALI wadogo 1,300, wakiwemo wafanyabiashara wa masoko na wasindikaji wadogo, wamenufaika na mradi INCLUCITIES katika kipindi cha miaka miwili ya utekelezaji wake katika Jiji la Mwanza(Wilaya ya Ilemela na Nyamagana) na Kisiwa cha Pemba.
Mradi huo ulilenga kuimarisha maendeleo ya kiuchumi jumuishi kwa kuwawezesha wajasiriamali kupata huduma za biashara,ujuzi,fursa za kifedha na masoko, hususani kwa wanawake na vijana,unaotekelezwa na shirika la TRIAS Tanzania chini ya Mpango Green and Smart Cities SASA wa Umoja wa Ulaya na Enabel,ulianza Julai 2024 na kufikia kilele chake Septemba 30, 2026.

Akizungumza Septemba 16,2026 wakati wa hafla ya kufunga mradi huo iliofanyika wilayani Ilemela mkoani Mwanza,Mkurugenzi wa shirika la TRIAS Afrika Mashariki Ritha Tarimo amesema,ili kuwa na uchumi imara hawawezi kuangalia biashara pekee, wanapaswa kuimarisha watu, biashara hizo na taasisi zinazo wakilisha kundi hilo,ambapo wajasiriamali wadogo na wasindikaji waliweza kupata mitaji na asilimia 86 walikuwa wanawake.
Tarimo amesema, kupitia mradi huo wanufaika wamejifunza kwamba kulinda mazingira na kujenga uchumi siyo lazima viwe vitu tofauti,kupitia kazi kwenye mnyororo wa thamani samaki,mwani pamoja na uchumi mzunguko wameanzisha kuona fursa ambazo zinaweza kuunganisha mazingira,biashara na kipato.
Ambapo wameona taka zinaweza kuwa malighafi, changamoto za mazingira zinaweza kutoa nafasi ya ubunifu na mzunguko wa kijani na buluu unaweza kuwa chanzo cha biashara,hii ni fursa ambayo inaendelea kufanyiwa kazi.
“Kupitia mradi huu tumeuunga mkono biashara zaidi ya 138 zenye uelekeo wa kukua,tumeunganisha wajasiriamali na maendeleo ya biashara,masoko, teknolojia,wadau wa uwekezaji na fursa na kuimarisha pamoja taasisi zinazowahudumia wanachama za TNCC, TWCC na ZNCC ambazo sasa zina mifumo ya kidigitali ya usimamizi wa wanachama,”amesema Tarimo na kuongeza:
“Tumepata kujenga uwezo siyo utegemezi,tumepata kujenga taasisi siyo shughuli za muda mfupi,tumekuwa tukifungua fursa ambazo zikiendelea kukua hata mradi ukiisha.Mafanikio hayapo kwenye namba,kuna mwanamke aliyepata mtaji,mjasiriamali aliyepata masoko na vijana waliogundua changamoto ya mazingira inaweza kuwa fursa ya biashara,kuna taasisi sasa ambazo zina uwezo mkubwa zaidi ya kuwahudumia wanachama wake,”.
Pia amesema,kuna faida kubwa kuendeleza walicho kijenga hata kama mradi unafika rasmi mwisho Septemba 30,2026 lakini biashara na vikundi havifungwi,taasisi haifungwi na mifumo walioiweka haifutwi na fursa walizobaini hazipotei,hivyo wanufaika hao wanapaswa kugeuza mafanikio hayo kuwa msingi wa hatua inayofuata.

Akiwasilisha taarifa kuhusu utekekalezaji wa mradi huo Mratibu wa Mradi wa shirika la TRIAS,Godfrey Kusekwa amesema,mradi umechangia kukuza uchumi wa kijani, uchumi mzunguko na uchumi wa buluu kupitia shughuli katika sekta za uvuvi, mwani, usimamizi wa taka na biashara nyingine zinazozingatia matumizi endelevu ya rasilimali.
Pia uliunda na kuimarisha vikundi 66 vya akiba na mikopo vya kijamii, ambavyo vimekusanya zaidi ya sh.milioni 417 kupitia akiba za wanachama, hatua inayosaidia kuongeza uwezo wa jamii kupata huduma za kifedha na kujenga ustahimilivu wa kiuchumi.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo,Mkuu wa Idara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Mkoa wa Mwanza Patrick Karangwa amesema,”Kuna usemi mmoja kwenye uchumi unasema kwamba uchumi wa kitaifa,ni muunganiko na mkusanyiko wa mtu mmoja mmoja.Tujipange kutumia maarifa,ujuzi na mitaji mlioipata kupitia mradi huo na kutobweteka badala yake muendeleze mlichokipata kwa manufaa yenu na uchumi wa nchi, kwani Serikali inapokea jitihada za mashirika ya maendeleo za kuwezesha wananchi,”.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo Mkurugenzi wa Kampuni ya FHT inayozalisha taulo za kike za muda mrefu Dkt.Idda Mihindi amesema,kupitia mradi huo umesaidia kununua vifaa katika kiwanda chaoashine kubwa za kusafisha bidhaa na kuongeza uzalishaji mara tano zaidi ya awali huku Sabina John amesema,kupitia mradi huo waliweza kuanzisha kikundi cha kusaidia na kukopeshana na sasa wamepiga hatua kwani walianza kukopeshana kila mmoja sh.50,000 lakini mpaka sasa wanauwezo wa kukopa sh.200,000 hadi sh.500,000.
Katibu Msaidizi wa Tanzania Women Chamber of Commerce(TWCC) Mkoa wa Mwanza Praxeda Mgyabuso alisema,kupitia mradi huo wanawake wamejengewa uwezo akiwemo yeye na ameweza kuanzisha biashara yake huku wajasiriamali wameweza kukuza biashara zao,kwa kujua na kuandaa mipango biashara na namna gani wataweza kufikia wadau wanaoweza kukuza biashara zao.

More Stories
Mixx, ZANGOF kuziwezesha Asasi za kiraia Zanzibar
Polisi Mwanza yafanyia kazi malalamiko ya wananchi
Wananchi Ilala wanaoishi mabondeni watakiwa kuhama