September 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kawaida: Ulinzi wa miundombinu usisubiri vyombo vya dola

Na Moses Ng’wat, Mbozi

WANANCHI wametakiwa kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu ya umma na kutosubiri vyombo vya ulinzi na usalama pekee pale inapojitokeza dalili za uharibifu au hujuma.

Wito huo umetolewa, Septemba 17, 2026, na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM) Taifa, Mohammed Kawaida, mara baada ya kukagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Songwe, kinachojengwa Kijiji cha Nsenya, Kata ya Hasamba, Wilaya ya Mbozi.

Kawaida yuko mkoani Songwe kwa ziara ya siku nne ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM, hususan miradi inayolenga vijana, ikiwemo wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya mradi huo, Kawaida amesema miundombinu hiyo haijengwi kwa ajili ya Serikali pekee, bali inalenga kuwasaidia vijana, kina mama, kina baba na wananchi kwa ujumla, hivyo wanapaswa kuilinda.

“Hii miundombinu haijengwi kwa ajili ya Serikali, bali inajengwa kwa ajili ya wananchi wote, hivyo akijitokeza mtu anayetaka kuiweka dosari au kuihujumu, tusisubiri vyombo vya ulinzi na usalama,” amesema.

Kawaida amesema jukumu la ulinzi na usalama ni la kila Mtanzania, akiwataka wananchi wa Mbozi kuwa walinzi namba moja wa miundombinu yote inayotekelezwa kwa ajili ya maendeleo yao.

Kwa mujibu wa Mthibiti Mkuu wa Shule, Wilaya ya Mbozi, Tusa Mwakajonga, mradi huo ulianza mwaka 2023 na unakadiriwa kugharimu Sh bilioni 7.36, huku ukihusisha ujenzi wa majengo 25, ikiwemo jengo la Utawala, Maktaba, Madarasa, Bwalo na Jiko, Karakana saba, Nyumba tano za watumishi na Mabweni manne.

Mwakajonga amesema hadi sasa mradi umefikia asilimia 76 baada ya kupokea Sh bilioni 5.02, huku ujenzi ukitarajiwa kukamilika Desemba 2026 na chuo kuanza kudahili wanafunzi katika fani mbalimbali Januari 2027.

Kwa upande wake, Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga, amesema kuanzishwa kwa chuo hicho ni hatua muhimu katika kubadili fikra za vijana kwa kuwawezesha kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia kujiajiri.