*Msisitizo elimu ya kupinga rushwa ianze darasa la tatu
*Wazazi na walimu washirikishwe kujenga kizazi cha waadilifu
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Tanga
SERIKALI mkoani Tanga imetaka mapambano dhidi ya rushwa yaanze kwenye ngazi ya chini kabisa ya elimu, ikiwamo shule za msingi kwa kuwafundisha watoto madhara ya rushwa na kuwajengea misingi ya uadilifu,uaminifu, uwajibikaji na uzalendo tangu wakiwa wadogo.
Hayo yameelezwa na Ofisa Elimu Mkoa wa Tanga, Emanuel Kisongo,kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt.Batilda Burian,wakati wa fainali ya mashindano ya Chemsha Bongo Zuia Rushwa 2026 mkoani Tanga, yaliyofanyika katika shule ya sekondari ya ufundi Tanga (Tanga Technical Secondary School),ambapo amesema,hatua hiyo ni muhimu katika kujenga kizazi kitakachokataa rushwa kama sehemu ya maisha na badala yake kusimamia haki,ukweli na maendeleo ya taifa.

Amesema elimu hiyo inapaswa kuanza mapema, akipendekeza wanafunzi waanze kufundishwa masuala ya kupinga rushwa kuanzia darasa la tatu, ili misingi ya maadili ijengwe kabla ya mtoto hajakua na kuingia katika mazingira mapana zaidi ya kijamii.
Kisongo amesema,watoto wana nafasi kubwa katika mapambano ya muda mrefu dhidi ya rushwa kwa kuwa elimu wanayoipata wakiwa wadogo inaweza kuwa sehemu ya misingi ya maisha yao ya baadaye.
Hivyo kuwafundisha watoto kuhusu rushwa hakupaswi kuishia katika kutaja maana yake, bali wanapaswa kuelewa madhara yake kwa jamii, uchumi, huduma za kijamii na maendeleo ya nchi.
Sanjari na hayo amesema,walimu wana wajibu wa kuwa vielelezo vya maadili kwa wanafunzi na mfano wa kuigwa na mtoto katika uadilifu,uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria, huku akisisitiza umuhimu wa kuwafundisha wanafunzi athari za rushwa katika maisha ya kila siku.
Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga, Ramadhan Ndwata amesema,mashindano ya Chemsha Bongo Zuia Rushwa 2026 ni sehemu ya mkakati wa kujenga kizazi chenye uadilifu kupitia elimu na kuwajenga kuwa raia watakaoweza kutambua,kukataa na kupinga vitendo vya rushwa wanapokutana navyo katika jamii.
Ndwata amewataka wazazi kushiriki katika malezi ya watoto na kushirikiana na shule pamoja na wadau wengine kuhakikisha elimu ya kupinga rushwa haiishii darasani.kwani familia ina nafasi kubwa katika kujenga au kuvunja misingi ya maadili ya mtoto.

Naye mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kisosora, Mariam Juma amesema,klabu hizo zimekuwa nyenzo muhimu katika kuwaelimisha wanafunzi kuhusu madhara ya rushwa kwa jamii na taifa hivyo amesisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa klabu hizoi ili kufikia wanafunzi wengi zaidi.

.

More Stories
Prof.Kabudi ahimiza matumizi teknolojia za kisasa katika uzalishaji
MWADETA yaomba kuongezwa walimu elimu maalumuÂ
Chongolo aitaka NIRC kukamilisha ugawaji wa Pampu za Umwagiliaji