April 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB yaahidi mikopo zaidi kuongeza mnyororo wa thamani zao la kahawa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Songwe

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege ameahidi kukiwezesha kifedha kiwanda cha kuchakata kahawa cha Mbozi Coffee Curing kilichopo mkoani Songwe ili ikiweze kuhudumia wakulima wengi wa zao hilo Nyanda ya Juu Kusini.

“Endepo kiwanda hicho kitawezeshwa kifedha ni matumaini makubwa ya TADB kuwa kitasaidia sana kuongeza thamani mnyororo wa zao la kahawa katika mikoa ya Nyanda ya Juu kusini mwa Tanzania,” amesema Nyabundege.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara yake akiwa amefuatana na watendaji wengine wa benki hiyo kwenye kiwanda hicho jana, Nyabundege amesema TADB itatoa fedha ilikuufanyia maboresho mradi huo ili kuinua soko la kahawa katika mikoa hiyo.

Ziara hiyo ambayo ilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya wateja Duniani, Nyabundege amesema yeye na timu yake wamejionea miradi inayofanywa na wadau katika mnyororo mzima wa thamani wa zao la kahawa kujua changamoto zao na namna benki itakavyoweza kusaidia ili kuongeza uzalishaji wenye tija kwa zao la kahawa na kuleta faida kwa mkulima na Taifa kwa ujumla wake.

“Benki ya kilimo imejipanga kuhakikisha inawafikia wadau wake ambao ni wakulima na wawekezaji kwenye mnyororo wa thamani za kilimo kwa kuwapatia mikopo itakayoweza kuboresha hali ya uzalishaji na kufanya wakulima kunufaika kupitia kilimo,” amesema Nyabundege.

Amesema amepata fursa ya kujifunza juu ya mnyororo mzima wa zao la kahawa hivyo kupitia na alichojifunza na kuona changamoto zilizopo wataendelea kujipanga ili kuhakikisha miradi inaendelezwa ili kuleta manufaa kwa wakulima nan chi kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Frank Nyabundege akikagua kahawa ikiwa inachambuliwa na Matrida Mwaitege (katikati), mfanyakazi wa kiwanda cha kukoboa kahawa, Mbozi Coffee Curing Company (MCCCO) iliyopo Mlowo, mkoani Songwe. Akishuhudia kulia ni Meneja Mkuu wa kiwanda cha MCCCO, Oscar Mvanda.

“Miradi kama hii inayokuwa kuwa soko la uhakika kwa mazao ya wakulima ni muhimu ipate mitaji ambayo itawawezesha kuendesha miradi yao na kumhakikisha mkulima soko la kudumu la mazao yake hali itakayopelekea maendeleo kwa wakulima na kukuza pato la taifa,”amesema Nyabundege

Ameeleza kuwa mikopo itakayotolewa kwa wawekezaji wa miradi ya viwanda itawawezesha kununua kahawa za wakulima moja kwa moja na wao baada ya kuchakata na kuuza wataweza rejesha mkopo na wao kupata faida jambo ambalo litasaidia sekta ya kilimo kuchangia sehemu kubwa katika pato la taifa.

“Tutaendelea kutoa mikopo kwa wakulima itakayowawezesha kupata mbegu bora, pembejeo za kilimo kwa wakati pamoja na zana bora za kilimo zitakazopeleka tija katika uzalishaji wa mazao bora yakayokubarika katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesema Nyabundege

Aidha, ametoa rai kwa wadau katika mnyororo mzima wa thamani wa zao la kahawa kutembelea ofisi za TADB zilizopo katika kanda mbali mbali hapa nchi na kupatiwa elimu na mafunzo ya uaandaji wa miradi ili waweze kupata mikopo itakayowawezesha kuanzisha na kuendeleza miradi yao hali itayopelekea nchi kupiga hatua kiuchumi.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mbozi Coffee Curing, Oscar Mvanda ameshukuru kutembelea na Mkurugenzi Mkuu wa TADB katika kiwanda chake na kupata nafasi ya kueleza changamoto zao za mtaji katika kuendelea mnyororo wa thamani wa zao la kahawa sambamba na kutengeneza soko la uhakika la zao hilo kwa wakulima.

“Kiwanda chetu kinafanya kazi na wakulima kupita vyama vya msingi vya ushirika (AMCOs) zaidi ya 70 ambavyo kila chama kinawakulima 50 utaona tunahudumia wakulima wengi sana hivyo tukiwezeshwa mtaji wa kuboresha kiwanda na kuweza kulipa wakulima kwa wakati tutakuwa tumechangia pakubwa kwenye kuleta maendeleo nchini,”amesema Mvanda

Uongozi wa TADB upo Nyanda za juu kusini wakitembelea wadau katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kubaini changamoto na mapendekezo katika kuboresha huduma zao ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya wateja Duniani.