May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

 NMB kupeleka huduma za kibenki vijiji 1,000 mwaka huu

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Zanzibar

Benki NMB imeanzisha mpango mkakati wa huduma za kibenki kwenye vijiji 1,000 nchini ambavyo havijawahi kufikiwa na huduma  zozote za kibenki lengo likiwa kuwasogezea wananchi huduma hiyo ili fedha zao ziwe sehemu salama.

Hayo yamesemwa Aprili 23, 2024 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa  NMB Ruth Zaipuna kwenye Mkutano Mkuu wa 38 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika mjini Zanzibar na kuongezeka kuwa benki hiyo imeongeza huduma za kibenki kwenye nyanja nyingi ikiwemo NMB Pesa.

Katibu Mkuu wa ALAT Taifa Mohamed Maje akisaini kitabu kwenye banda la NMB katika Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa, Zanzibar. Kulia ni Ofisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali, Alfred Shao.

Ambapo ameeleza kuwa kwa miezi miwili ya kwanza, wamefungua akaunti zaidi ya 100,000 huku lengo lao mwaka huu ni kufungua akaunti milioni 1.5 ili kuwafikia Watanzania wengi katika sekta rasmi ya kibenki.

“NMB tunaendelea kusogeza huduma zetu kwa wananchi,tumezindua mkakati wetu wa kibenki vijijini yaani Rural Bank,kupitia package hiyo lengo letu kwa mwaka huu pekee ni kupeleka huduma za kibenki kwenye vijiji 1,000 visivyokuwa na huduma za kibenki na kwa kuanzia tutapeleka huduma ya mawakala,”ameeleza Zaipuna.

Amesema benki hiyo imekua mshirika  wa karibu  kupitia halmashauri  hapa nchini ambapo ushirikiano huo umejikita katika maeneo mbalimbali ikiwemo utoaji wa huduma za kifedha, ukusanyaji wa mapato kwa halmashauri zote,  kuboresha miundombinu ya elimu, afya, kilimo, barabara na kuchangia katika kutunza mazingira, na vyanzo vya maji huku lengo likiwa ni kuhakikisha  kunakuwa na utoaji wa huduma bora kwa Watanzania. 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa ALAT.

“Katika kipindi cha miaka miwili (2022 – 2023), benki yetu imetoa zaidi ya sh. bilioni saba kwenye sekta ya elimu, afya, mazingira, kilimo na uokoaji kipindi cha maafa katika kutekeleza sera yake ya kurudisha sehemu ya faida kwa jamii na  mwaka jana tuliboresha jengo la Wazazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, na mpaka sasa tayari sh. milioni 350 zimeshatumika,”ameeleza na kuongeza kuwa 

“Mwaka uliopita benki iliweka historia kwa kutengeneza faida ya sh. bilioni 542 baada ya kodi,kutokana na faida na kutambua umuhimu wa kuwa na maendeleo endelevu  NMB ilitangaza rasmi kutenga sh. bilioni 5.4 kwa ajili ya kurejesha kwa jamii (Corporate Social Investment– CSI),tuna programu ya ufadhili wa masomo ya Nuru Yangu Scholarship and Mentorship, ambapo wanafunzi wenye ufaulu mzuri na wanaotoka familia zenye uhitaji, tunawapa ufadhili wa kusoma elimu ya juu,” amesema Zaipuna.

Waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa maofisa wa Benki ya NMB, baada ya kutembelea banda la NMB kwenye Mkutano Mkuu wa ALAT

Amesema wanalipa gharama zote za msingi ikiwa ni pamoja na ada ya masomo, vifaa vya shule, usafiri, wanawapa kompyuta, bima ya afya na pia wanawapa mafunzo ya vitendo na ushauri, ili kuwajenga kuwa vijana wenye uadilifu na uzalendo kwa nchi  na mpaka sasa, wana wanafunzi 130 chini ya program hiyo na wako wanasoma vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini.

Zaipuna amesema katika kushiriki kufanikisha miradi ya kimkakati kama ujenzi wa barabara, madaraja, Reli ya Kisasa  (SGR) na mingine, benki imekua ikitoa masuluhisho na  dhamana kwa wakandarasi wa ndani na  nje. 

Ambapo impetoa dhamana kwa wakandarasi zaidi ya 580 wanaotekeleza miradi ya TARURA yenye thamani ya sh. bilioni 49 kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa miundombinu.

“Benki pia imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuzihudumia sekta zote na kwa zile za kimkakati tumekua tukiongeza nguvu  zaidi,mfano sekta ya kilimo tumeongeza mikopo kutoka sh. bilioni 557 mwaka 2020 mpaka sh. trilioni 1.6 mwaka 2023,hivyo hivyo kwa sekta kama za nishati, uzalishaji na biashara.

Waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa (wa pili kulia) akizungumza mara baada ya kukaribishwa kwenye banda la NMB na Ofisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali Alfred Shao (wa tatu kushoto)

Aidha ameeleza kuwa benki hiyo imeendelea kuongeza ujumuishwaji wa Watanzania wengi zaidi kwenye sekta rasmi ya kifedha hususani waliopo vijijini ambapo kupitia huduma hiyo mpya ya  NMB Pesa wamerahisisha masharti ya kufungua akaunti hiyo ambapo kwa sh. 1,000 tu, Mtanzania anaweza kufungua akaunti.

“, Akaunti hii haina makato ya mwezi na  mteja atapewa uwezo wa kujiunga na NMB Mkononi kurahisisha miamala yake na baada ya kujenga miamala,atakuwa na uwezo wa kukopa hadi sh. 500,000 kwa simu, bila kufika tawini, kwa kutumia huduma ya MshikoFasta,” amesema Zaipuna. 

Hata hivyo ameeleza kuwa kwa kipindi cha miaka minane (8) wamelipa kodi ya zaidi ya sh. trilioni 1.8 ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliwatambua kama washindi wa jumla kitaifa kama mlipa kodi bora na mkubwa zaidi Tanzania (Sekta zote), hii ikiwa ni mara ya pili na taasisi bora inayolipa kodi kwa hiari kwa kuzingatia misingi na kanuni bora za ulipaji kodi (Most Compliant Tax Payer) na mshindi wa kwanza mlipa kodi mkubwa zaidi katika kundi la taasisi za fedha nchini (mara ya tatu mfululizo).

Baadhi ya Maofisa wa Benki ya NMB wakiwa kwenye banda la benki hiyo katika Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa unaofanyika kwa siku tatu Zanzibar