May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndejebi : Serikali inafanyia maboresho sheria ya fidia kwa wafanyakazi


 NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, KIGOMA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Deogratius Ndejembi amewahakikishia Majaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na wadau wengine kuwa, Serikali inayachukulia kwa uzito mkubwa maoni yao kuhusu kuboresha baadhi ya vifungu vya sheria ya fidia kwa wafanyakazi wanaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo wakati wa kufunga kikao kazi kati ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania – Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kati ya Magharibi, Kamishna wa Kazi, Menejimenti ya Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Aprili 20, 2024 Mkoani Kigoma.

“Tayari maoni mliyotoa ya kuboresha kifungu cha 39 (2) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263] kilichoweka ukomo wa muda wa kuwasilisha madai bila kutoa wigo wa kupokea madai hayo iwapo kuna sababu za msingi za kucheleweshwa kwake, tumeshayafanyia kazi na maboresho hayo kuwa sehemu ya muswada wa marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii uliosomwa Bungeni kwa mara ya kwanza tarehe 15 Februari 2024.” Amefafanua.

Aidha Mhe. Ndejembi amesema, WCF kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Hifadhi ya Jamii Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), wanaendelea na uchambuzi wa maboresho ya sheria ya fidia kwa wafanyakazi ambayo yalitolewa na Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi.

Awali akifungua kikao hicho Aprili 19, 2024, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamisi Juma, amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema lengo la vyombo vyote vya dola ni ustawi wa wananchi, WCF kama chombo cha serikali inagusa ustawi wa wananchi.

“WCF ni Mfuko unaogusa ustawi wa wananchi, kwasababu unaweza kuwa unamtegemea mama, kaka, bahati mbaya akapata ajali akafariki, hapa ustawi wa familia unaweza kutoweka, kama hakuna Mfuko unaoweza kubeba hilo jukumu, kwa hivyo huu Mfuko ni muhimu mno mno.” Amebainisha Mhe. Profesa Juma.

Aidha Mhe. Profesa Juma amehimiza umakini na uadilifu katika utekelezaji wa sheria hiyo ya Fidia kwa Wafanyakazi.

“Ukosefu wa umakini, udanganyifu vyote vimechangia kuua mifuko ambayo ilikuwa na malengo mazuri sana. Tusipokuwa waangalifu, mfuko huu wa WCF vile vile unaweza kukumbana na tatizo hili. Tukielewa vizuri mantiki ya kuanzishwa mfuko huu tutaufanya uwe endelevu na himilivu,” amesema.

Aidha Mhe. Jaji Mkuu ameipongeza WCF kwa kupiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu yake na kukumbusha umuhimu wa mifumo ya taasisi za umma kusomana ili kurahisisha utoaji wa huduma.

“Ifike mahala mfanyakazi anapowasilisha madai yake WCF, mfumo mzima uwe unaelewa kwamba mfanyakazi fulani amepata ajali kazini au amefariki. Mifumo ya serikali ikiweza kutambuana pia itasaidia sana kuziba mianya ya udanganyifu.” Alisisitiza.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Emmanuel Humba, amesema Bodi na Menejiment ya WCF wataendelea kushirikiana na Mahakama

Akizungumzia kuhusu nia ya kikao kazi hicho, Bw. Humba alibainisha kuwa pamoja na kwamba jukumu la kulipa fidia limekasimiwa kwenye Mfuko, Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi imeweka utaratibu na vyombo vya kushughulikia madai ya wanufaika pale wanapokuwa hawajaridhika na fidia iliyolipwa au maamuzi ya Mfuko yanayokinzana na matarajio yao.

“Kutokana na hitaji hili muhimu la kisheria, Bodi ya Wadhamini ya WCF, Menejimenti ya Mfuko pamoja na Watendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi waliona kuna hitaji la kufanya vikao kazi kwa lengo la kubadilisha uzoefu, kujenga uelewa wa pamoja na kubainisha maeneo ya sheria yanayohitaji maboresho kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kutekeleza Sheria hiyo.” Alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma ameeleza kuwa ushirikiano baina ya Mfuko na Mahakama ni muhimu kwa vile kuna maeneo mengi ambayo Mfuko unakutana na Mahakama katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Sisi kama WCF shughuli zetu hazikamiliki bila ya uwepo wa shughuli za Mahakama. Kwa mfano katika kushughulikia masuala yanayohusu mirathi, Mfuko hutegemea maamuzi ya Mahakama.” Alisema Dkt. Mduma

Alisema kuwa Mfuko umefanya vikao kazi vitano ambavyo vimefanyika baina ya Mahakama, WCF na Watendaji wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Deogratius Ndejembi (kulia), akipokea tuzo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, baada ya kufunga kikao kazi kati ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania – Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kati ya Magharibi, Kamishna wa Kazi, Menejimenti ya Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Aprili 20, 2024 Mkoani Kigoma. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, WCF, Bw. Emmanuel Humba.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Deogratius Ndejembi, akifunga kikao kazi kati ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania – Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kati ya Magharibi, Kamishna wa Kazi, Menejimenti ya Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Aprili 20, 2024 Mkoani Kigoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Deogratius Ndejembi, akifunga kikao kazi kati ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania – Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kati ya Magharibi, Kamishna wa Kazi, Menejimenti ya Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Aprili 20, 2024 Mkoani Kigoma.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, WCF, Bw. Emmanuel Humba, akizungumza wakati wa kikao hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, akizungumza mwanzo mwa kikao hicho. 
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, akielezea historia ya viao kazi baina ya Mfuko na Mahakama. 
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho
Mhe. Ndejembi, akizunguzma jambo na Dkt. Mduma.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho

 Mhe. Aziza Iddi Swedi, Jaji Mwenye dhamana ya Divisheni ya Kazi Mahakama Kuu, Zanzibar, akieleza uzoefu wa sharia inayosimamia masuala ya fidia kwa wafanyakazi huko Zanzibar.

Mmoja wa washiriki wa kikao hicho Mhe. Jaji Abdi Kagomba, akichangia mjadala kuhusu sheria ya fidia kwa wafanyakazi.