Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
ZAIDI ya wananchi 34,000 wa kata za Bugogwa,Sangabuye,Kahama na Shibula wilayani Ilemela mkoani Mwanza,wameanza kunufaika na mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji katika chanzo cha maji cha Igombe-Kabangaja,ambao ulizinduliwa rasmi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 Wazo Mwang’onda.
Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA),kwa kushirikiana na Shirika la Maji la Uholanzi(Vitens Evides International-VEI),wenye thamani ya sh.milioni 585 ambao umekamilika kwa asilimia 100 ukilenga kuongeza ubora na upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi wa maeneo hayo.

Akitoa taarifa ya mradi huo kwa kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,Agosti 11,2026 wakati wa uzinduzi wa mradi huo,Msimamizi wa miradi MWAUWASA Mhandisi Nuhu Said amesema,utekelezaji ulianza Oktoba 01,2024 na umekamilika Juni 30 2026 kwa asilimia 100.
Mhandisi Said amesema,kazi zilizotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa nyumba ya mtambo wa kuchuja maji, ununuzi na usimikaji wa tanki la mita za ujazo 100,ununuzi na usimikaji wa pampu 2 zenye ukubwa wa mita za ujazo 50 kwa saa, ulazaji wa bomba la 200 mmm GS urefu wa mita 12 na bomba la 100mm ST la kupeleka maji kwenye tenki pamoja na ujenzi wa choo na uzio.
“Mradi huu umeleta manufaa kwa kuongeza ubora wa maji kuwa kwenye kiwango cha juu ambayo inatupatia uwezo wa kuandika maandiko mradi ili kuweza kupata miradi ya kupanua mitandao ya maji na maunganisho kwa wateja.Pia mradi umetoa ajira za muda kwa vijana 25,”amesema Mhandisi Said.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 Wazo Mwang’onda amesema,mradi huo ni muhimu unaogusa maisha ya wananchi moja kwa moja kwa kuwa utaongeza upatikanaji wa majisafi na salama na hivyo kuchangia kuboresha afya na ustawi wa jamii.
Hata hivyo Mwang’onda ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo,hivyo aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Maji na MWAUWASA, kwa kuendelea kutekeleza miradi muhimu ya maji inayolenga kutatua changamoto za wananchi na kuboresha huduma za kijamii.
“Ahadi ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kumtua mama ndoo kichwani,niwaombe wananchi tuendelee kuitunza miradi na miundombinu hii ya maji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,”amesisitiza Mwang’onda.

Naye mmoja wa wananchi wa Wilaya ya Ilemela Agnes Lucas amesema,ni jambo jema mradi huo kuzinduliwa hivyo aliomba mamlaka husika kuhakikisha huduma inawafikia wananchi wote kama ilivyo kusudi la mradi.
Vilevile MWAUWASA inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha uwekezaji katika miundombinu ya maji unaoendelea kuleta matokeo chanya na kuboresha maisha ya wananchi.


More Stories
Mradi wa mageuzi tansia ya maziwa kuongeza uzalishaji
Yanga yatwaa Ngao ya Jamii ,Simba chali
Msajili wa Hazina, Fitch Ratings watathmini mageuzi ya taasisi za ummaNa Mwandishi wa OTRDar es Salaam