
Na Israel Mwaisaka, Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) mkoani Rukwa kuoanisha mipango na miradi yao na vipaumbele vya taifa, hususan Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili kuongeza mchango wao katika maendeleo endelevu.
Makongoro ametoa wito huo jana Agosti 11, 2026 wakati akifungua Jukwaa la Mwaka la NGOs Mkoa wa Rukwa, akibainisha kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa mashirika hayo katika sekta za afya, elimu, kilimo, lishe, maji, mazingira, uwezeshaji wa wanawake na vijana, pamoja na ulinzi wa watoto na makundi maalum.
Amesema Dira ya taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga uchumi shindani unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia, hivyo NGOs zinapaswa kuelekeza miradi yao katika kuongeza uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na malighafi, kuboresha huduma za jamii, kuwawezesha wananchi kiuchumi na kujenga uwezo wa jamii kujitegemea.
Aidha, amezitaka NGOs kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya shughuli za kitaifa za Mbio za Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika mkoani Rukwa kuanzia tarehe 8 hadi 14 Oktoba 2026, ikiwemo Wiki ya Vijana, kilele cha Mbio za Mwenge na kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kutoa elimu, kushiriki shughuli za mazingira, afya, lishe na uwezeshaji wa vijana, pamoja na kuchangia rasilimali.
Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Makongoro amezitaka NGOs kushirikiana na Serikali katika maandalizi na hatua za kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa, mafuriko, uharibifu wa miundombinu, magonjwa ya mlipuko na athari katika uzalishaji wa kilimo.
Ameziagiza pia kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika hatua zote za utekelezaji wa miradi, kuanzia kubaini mahitaji, kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini, akisisitiza kuwa ushiriki huo huimarisha umiliki na uendelevu wa miradi.
Katika kuimarisha utawala bora, amezitaka NGOs kuzingatia uwazi, uwajibikaji na uratibu na Serikali, pamoja na kuwasilisha kwa wakati taarifa za utekelezaji wa miradi, mafanikio, changamoto na matumizi ya rasilimali.
Pia amesisitiza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na NGOs zinazotekeleza shughuli zao kwa kuzingatia sheria, sera, miongozo na vipaumbele vya Taifa.
Na amezitaka NGOs kujiepusha na masuala ya kisiasa na kubaki katika majukumu waliyojisajili kuyatekeleza, akibainisha kuwa vyama vya siasa vina wajibu wa kushughulikia shughuli za kisiasa.

More Stories
Monde Selection yaitunuku SBL tuzo ya Gold Quality
Kabudi aagiza ujenzi wa Ofisi kukamilika kwa wakati
Serikali yakabidhi Pampu 52 za umwagiliaji kwa wakulima