April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB yapongezwa kutoa bil.3.3/- kufufua kiwanda cha pamba Geita

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Geita

WADAU katika mnyororo wa thamani wa zao la pamba mkoani Geita wameishukuru Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kutoa mkopo kiasi cha sh. bilioni 3.3 kwa kiwanda cha kuchakata zao hilo cha Masumbwe Ginnery kilichopo kanda ya ziwa, ambapo zaidi ya wakulima 12,000 wa zao hilo kutoka vyama 84 vya msingi vya ushirika (AMCOS) wamenufaika kwa kuuza pamba yao kutokana na uwepo wa kiwanda hicho.

Wakulima wameanza kunufaika na zao hilo kutokana na uwepo wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha (MBCU LTD) ambacho kipo katika kata ya Nyakasaluma, Masumbwe wilayani Mbogwe Mkoani Geita.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya kukua kwa kilimo cha pamba, Mwenyekiti wa Chama hicho, Benadict Bulugu ametoa shukrani zake kwa TADB kwa kuwezesha kuwepo kwa kiwanda hicho ambacho kimekuwa mkombozi kwa wakulima wengi kanda ya ziwa.

“Kiwanda hiki kina uwezo wa kuchambua pamba marobota 240 kwa siku na kutoa huduma ya uchakataji wa zao hilo kutoka kwa wakulima hivyo kufanya uhitaji wa pamba kuongezeka na hivyo kuhamasisha wakulima wengi kuzalisha pamba kwa tija,” amesema Bulugu

Amesema changamoto inayowakabili katika uzalishaji ni kukatika kwa nishati ya umeme mara kwa mara, na hivyo kuiomba serikali kuboresha huduma hiyo ambayo ni muhimu ili uzalishaji wao ufanyike kwa ufanisi zaidi na kunufaisha watu wengi.

“Wanachama wa zao hili wameweza kunufaika na ongezeko la bei kutoka sh. 1,050 hadi kufikia sh. 1,800 hii ni kutokana na uwekezaji uliofanywa na ushirika kupitia mkopo kutoka TADB,” amesema Bulugu

Zao la pamba

Ameeleza kuwa ongezeko la bei hiyo limekuwepo baada ya chama hicho kuanza kununua malighafi hiyo kwa wakulima vijijini waliopo katika wilaya ya Mbogwe, Bukombe, Geita, Nyang’wale, Biharamulo na Kasulu, ambao wameanza kuonja utamu wa zao la pamba, ambalo kimsingi katika miaka ya nyuma, bei ya zao hilo ilikuwa ikiwakatisha tama wakulima.

Kaimu meneja wa chama kikuu cha ushirika (MBCU L.T.D) David Magai, amesema mwamko wa wakulima hivi sasa wa kulima zao hilo uko juu baada ya kiwanda kuanza kufanya uzalishaji kwa kuelekeza macho yake maeneo ya vijijini kununua zao hilo.

Tunatarajia kuwa msimu ujao wa kilimo tutapata malighafi nyingi kutoka kwa wakulima kwa wegi watahamasika kulima kutokana na ongezeko la bei na uhakika wa soko ambalo ni uwepo wa kiwanda,” amesema Magai

Matokeo hayo vilevile yanahusisha ongezeko la ajira zaidi kwa watumishi 168, wakiwemo vibarua 140 na watumishi 28 wenye ajira za kudumu.

Mkuu wa wilaya ya Mbogwe mkoani Geita Charles Kabeyo, ameishukuru serikali ya awamu ya sita kupitia benki ya TADB kwa kutoa fedha za mkopo kwa kukikopesha kiwanda hicho zaidi ya shilingi bilioni 3.3, kwa lengo la kukufua kiwanda hicho na sasa kimeanza kutoa huduma ya uchakataji wa pamba.

“Msimu uliopita kupitia kiwanda hicho, kimeweza kununua kilo za pamba milioni 1.5 na hivyo nawaomba wakazi wa wilaya hiyo kuendelea kulima pamba kwa wingi zaidi ukizingatia ni zao la kibiashara na kwamba soko lipo,” amesema Bw.Kabeyo

Kaimu Mkurugenzi wa mipango, sera na utafiti wa benki hiyo Mzee Kilele, amesema kwa kuwa benki hiyo ni benki ya kisera ya serikali itaendelea kuhakikisha zao la pamba linainuka nchini ikiwa ni pamoja na kuliongezea thamani, ili kuendelea kuimarisha thamani yake katika soko la dunia.