*Yatoa milioni 349 kwa kikundi cha Ukwavila
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Mbarali
SERIKALI imeendelea kuwawezesha mitaji vijana ambapo imetoa mkopo wa sh.milioni 349 kwa kikundi cha vijana cha Ukwavila kinachojishughulisha na shughuli za kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.
Mkopo huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi yenye thamani ya sh bilioni 200 iliyotolewa na Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuongeza fursa za ajira,kuimarisha ujasiriamali na kuinua uchumi wa vijana nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana,Dkt.Joel Nanauka, akizungumza juzi wakati wa hafla ya uzinduzi wa utoaji wa mikopo ya uwezeshaji kwa vijana,mkoani humo,alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupata mitaji itakayowawezesha kuanzisha na kukuza miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo kilimo,mifugo, uvuvi,viwanda vidogo na biashara, ili kuongeza ajira na kipato kwa vijana.
Dkt.Nanauka alisema,mkopo huo kwa kikundi cha Ukwavila utasaidia kuongeza uwezo wa vijana hao katika uzalishaji wa kilimo kwa kutumia mbinu za kisasa, kuongeza thamani ya mazao na kupanua masoko ya bidhaa zao, hatua itakayochangia ukuaji wa uchumi wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla.
Pia aliwataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, kusimamia miradi yao kwa uwajibikaji na kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili fedha hizo ziendelee kuwafikia makundi mengine ya vijana wenye uhitaji.
Hata hivyo Programu ya Taifa ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi ya sh.bilioni 200 inaendelea kutekelezwa na Ofisi ya Rais,Maendeleo ya Vijana kwa lengo la kuwawezesha vijana hapa nchini wenye miradi yenye tija kupata mitaji nafuu, kuongeza uzalishaji,kuibua ajira mpya na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.

More Stories
Mwalimu VETA abuni vifaa kusaidia afya na elimu
Wananchi kuchangia saruji ujenzi barabara
Serikali yaweka mazingira rafiki kuvutia uwekezaji sekta ya elimu