

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online
MWALIMU wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Tanga, Yusauf Mkahalla, amewasilisha ubunifu wa kifaa cha mbao cha kupimia mapigo ya moyo wa mtoto akiwa tumboni mwa mama pamoja na kalamu za maandishi ya nukta nundu (Braille) kwa ajili ya watu wenye uoni hafifu na wasioona, akisema lengo ni kupunguza gharama za vifaa vinavyoagizwa kutoka nje na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa Watanzania.
Mkahalla alitoa kauli hiyo alipozungumza katika banda la VETA kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), akieleza kuwa taasisi hiyo imekuja na bunifu mbalimbali zinazotokana na rasilimali za ndani kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya na elimu jumuishi.
Alisema kifaa hicho cha kupimia mapigo ya moyo wa mtoto tumboni, maarufu kama fetoscope ya mbao, kimebuniwa baada ya kubaini kuwa zahanati, vituo vya afya na hospitali nyingi nchini zinahitaji vifaa vya aina hiyo, huku vya kuagiza kutoka nje vikigharimu fedha nyingi.
“Baada ya kuona Serikali imejenga zahanati, vituo vya afya na hospitali nyingi, tuliona kuna umuhimu wa kutumia rasilimali zilizopo nchini kutengeneza kifaa hiki ili kupunguza gharama zisizo za lazima na kuongeza upatikanaji wa huduma,” alisema Mkahalla.
Aliongeza kuwa hatua inayofuata ni kufuata taratibu za mamlaka husika ili kifaa hicho kipate ithibati na kibali cha kutumika rasmi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Mbali na kifaa hicho, alisema VETA pia imebuni kalamu za maandishi ya nukta nundu kwa ajili ya watu wenye uoni hafifu na wasioona, akisisitiza kuwa elimu ya ufundi stadi ni fursa kwa kila mtu bila kujali hali yake.
“Ndugu zetu wenye changamoto za uoni nao wana ndoto zao. Ni wajibu wetu kuhakikisha wanapata vifaa vinavyowawezesha kujifunza na kutimiza ndoto hizo. Tunawakaribisha VETA kwa sababu vifaa hivi ni vyao na vinapatikana kwa gharama nafuu,” alisema.
Alifafanua kuwa kalamu hizo tayari zimefanyiwa majaribio na watumiaji wenyewe na zimeonekana kufaa, huku VETA ikiendelea kuzalisha vifaa hivyo kwa lengo la kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa bei nafuu.
Mkahalla alisema hadi sasa ubunifu huo haujakumbana na changamoto kubwa, huku VETA ikiendelea kuboresha bidhaa zake ili ziweze kukidhi mahitaji ya soko na kuchangia maendeleo ya sekta za afya, elimu na viwanda nchini.

More Stories
Serikali yaendelee kuwawezesha mitaji vijana
Wananchi kuchangia saruji ujenzi barabara
Serikali yaweka mazingira rafiki kuvutia uwekezaji sekta ya elimu