Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kutumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kama jukwaa la kutangaza bidhaa zinazozalishwa visiwani, ubunifu wa wajasiriamali pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji.
Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Zanzibar ndani ya maonesho hayo.
Mahmoud amesema serikali inaendelea kuwahamasisha wazalishaji, wafanyabiashara na wajasiriamali kushiriki kikamilifu katika maonesho ya biashara ili kupanua masoko ya bidhaa na huduma zao ndani na nje ya nchi.

Amesisitiza kuwa ubora wa bidhaa, vifungashio vya kisasa na utoaji wa huduma bora ni mambo muhimu yatakayowezesha bidhaa za Zanzibar kushindana katika soko la kikanda na kimataifa.
Aidha, amesema licha ya Zanzibar kuwa na eneo dogo kijiografia, ina uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa na huduma zenye ushindani. Ameeleza kuwa uwekezaji katika rasilimali watu, ubunifu na teknolojia utaendelea kuimarisha uchumi wa visiwa hivyo, kuongeza ajira na kufungua fursa zaidi za biashara kwa wananchi.

Mahmoud amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwawezesha wazalishaji kushiriki katika masoko ya kikanda na kimataifa, ikiwemo Soko la Afrika Mashariki na Soko Huru la Afrika (AfCFTA).
Pia amewakaribisha wananchi kutembelea banda la Zanzibar katika Maonesho ya Sabasaba kujionea bidhaa, huduma na fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi za serikali pamoja na sekta binafsi.



More Stories
TCAA yaimarisha dawati huduma kwa Wateja
Mtanzania Avith Philip ang’ara Orodha ya Wajasiriamali 100 Bora Afrika
Mwalimu VETA abuni vifaa kusaidia afya na elimu