April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Muhimbili yapokea mashine ya kuchunguza saratani ya matiti

Na Irene Clemence, Timesmajira Online,Dar

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili(MNH) imepokea mashine maalumu Mammography aina ya Senographe Pristina 3D kwa ajili ya kufanya uchuguzi wa saratani ya matiti.

Pia mashine hiyo itatumika katika kuwafundishia wataalam na kufanya tafiti mbalimbali.

Akizungumza katika hafla ya kupokea mashine hiyo Aprili 17, 2024 Dkt. Hamad Nyembea wakati akimuwakilisha Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema takwimu za kidunia zinaonesha wanawake milioni 2.3 wanagundulika kuwa na saratani ya matiti kila mwaka.

“Hapa nchini wanawake 42,000 kila mwaka wanagundulika kuwa na saratani hiyo huku wanaofika kwenye vituo vya afya kupata matibabu ni asilimia 38 tu”,amesema Nyembea.

Aidha amesema ujio wa mashine hiyo unaonesha ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Marekani na kuwezesha kukuwa kwa teknolojia katika sekta ya afya.

Huku ameeleza kuwa kwa sasa saratani ya shingo ya kizazi ndio inasumbua nchini lakini tayari jitahada zinaendelea kufanyika ila kuhakikisha inaisha.

Pia ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika sekta hiyo huku akitoa rai kwa watendaji kuhakikisha wanaitunza mashine hiyo na kuhakikisha inafanya kazi iliyokusudiwa.

Katika hatua nyingine alitoa wito wanawake kuwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti ili waweze kupata tiba ya haraka pindi wanapogundulika na tatizo hilo kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospital ya Taifa ya Muhimbili Profesa Mohamed Janabi
amesema mashine hiyo wameipokea kwa ukarimu wa Serikali ya Marekani kupitia Jumuiya ya Radiorojia ya Amerika Kaskazini (RSNA )na GE health Care .

Amesema mashine hiyo ni ya kisasa zaidi na ya kwanza ya aina yake kusimikwa katika hospitali ya Muhimbili na inauwezo wa kufanya kazi za huduma za kichuguzi za kawaida na kibobezi za matiti.

“Saratani ya matiti ni tatizo kubwa sana nchini Tanzania ambapo takwimu zinaonesha kuwa hii ni saratani ya pili Kwa wanawake katika nchi yetu na inaendelea kuongezeka inawezekana ugonjwa huu kudhibitika na kutibika kabisa ikiwa ugunduzi wake utafanyika mapema,”amesema.

Amesema bado kuna chagamoto kubwa ya wagonjwa wapya wa saratani kufika hospitali ambapo kila mwaka inakadiriwa ni asilimia 38 tu ndio wanao fika kwa ajili ya matibabu.

Amesema kupitia mashine hiyo itawezekana kufanya utambuzi wa mapema na kuokoa maisha ya wanawake wengi.

“Hospitali ya Muhimbili ni mwanga wa matumani kwa wengi tunakadiria walau si chini ya wagonjwa 2000 au 2400 kwa mwaka wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja kwa kupimwa na mashine hii ya kisasa Pristima 3D,”.

Naye Mwakilishi wa kitengo cha biashara kutoka GE Healthcare, Guillaume Fusari amesema ukosefu wa elimu kuhusu saratani ya matiti ndio inapelekea ongezeko la ugonjwa huo ambapo usababisha vifo hivyo ni muhimu kuwawezesha wanawake ili kupunguza idadi ya vifo.

Amesema ukosefu wa elimu bado ni chagamoto na sababu ya wanawake kuugua ugonjwa huo.