April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia apeleka magari kuhudumia wagonjwa Kaliua

Na Allan Vicent, TimesmajiraOnline, Kaliua

RAIS Samia Suluhu Hassan amepelekea magari mawili ya kuhudumia wagonjwa katika majimbo mawili yaliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora ili kuboresha utoaji huduma za dharura kwa wagonjwa.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Jerry Mwaga, alipokuwa akizungumza na TimesmajiraOnline, ofisini kwake jana, ambapo alieleza kuwa magari hayo yamekuja wakati mwafaka, kwani walikuwa na uhitaji mkubwa wa magari ya kuhudumia wagonjwa.

Amemshukuru Rais kwa kujali ustawi wa wakazi wa Wilaya hiyo na kuwapelekea magari hayo ambayo tayari yameanza kuhudumia wajawazito na wagonjwa wengine wanaohitaji huduma ya haraka katika hospitali kubwa.

“Magari haya yatasaidia kuokoa uhai wa akinamama wajawazito na wananchi wengineo wanaohitaji kusafirishwa haraka kwenda kwenye vituo vya afya au hospitali kubwa kupata huduma za afya,” amasema.

Mwaga amefafanua kuwa gari moja linatoa huduma katika Hospitali ya Wilaya hiyo ambayo ipo katika Jimbo la Kaliua na la pili lipo katika Kituo cha Afya Ulyankulu kwa ajili ya kuhudumia wakazi wa Jimbo la Ulyankulu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Japhael Lufungija amemshukuru Rais kwa kuendelea kuwapatia mabilioni ya fedha ili kuharakisha utekelezaji miradi ya wananchi na kuboreshwa huduma za jamii.

Amesema kuwa katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024 wamepokea zaidi ya sh bil 1.2 kwa ajili ya ukamilishaji zahanati za Mtapenda, Ulanga na Usinga na kununua vifaa tiba vya kutosha kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati.

Ameongeza kuwa pia wamepokea zaidi ya sh mil 156 za Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya utekelezaji miradi ya wananchi katika Majimbo hayo mawili ya Kaliua na Ulyankulu, vikao vya maamuzi ya matumizi ya fedha hizo vitakaa muda si mrefu.

Lufungija alibainisha kuwa halmashauri inaendelea kukamilisha miradi ya ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za msingi Kashishi, Kazaroho na Seleli kupitia programu ya SWASH ambapo walipokea zaidi ya sh mil 176 kwa kazi hiyo.

Aidha ameongeza kuwa wamepokea zaidi ya sh mil 600 kupitia programu ya SEQUIP kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari Sasu na sasa imekamilika kuanza kupokea wanafunzi.

Aidha kupitia programu hiyo walipokea kiasi cha sh mil 117.5 kwa ajili ya ukamilishaji vyumba vya madarasa na maabara katika shule za sekondari Dkt John Pombe Magufuli, Konanne, Mwongozo, Kazaroho na Seleli.

Ameongeza kuwa kupitia Programu ya Lipa kwa Matokeo (EP4R) walipokea sh mil 35.2 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za Wachawaseme, Ibambo, Mwangaza na Kangeme.

Aidha kwa upande wa Programu ya Elimu bila malipo alisema walipokea zaidi ya sh mil 400 ambapo sh mil 225.5 ni za elimu ya msingi na sh mil 183.4 ni za shule za sekondari.