May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU kuzuia vitendo vya rushwa kwa elimu ya usimamizi,matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Mkoa wa Mwanza,katika kuzuia vitendo vya rushwa kwenye miradi ya maendeleo,mkakati uliopo ni kutoa elimu kwa wananchi kusimamia matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa na serikali kutekeleza miradi hiyo.

Pia,katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka 2023/24, itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuchunguza makosa ya rushwa na kuwachukulia hatua watakaojihusisha na vitendo hivyo kwa mujibu wa sheria.

Kauli hiyo imetolewa Aprili 29,2024 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza,James Ruge wakati akitoa kwa waandishi wa habari, taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo katika kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu.

“TAKUKURU Mwanza inatoa wito kwa wananchi kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika maeneo yao,kwa pamoja tuzie na kukemea vitendo vya rushwa katika maeneo ya kupata huduma kwa kuwa ni jukumu letu sote wananchi,”amesema.

Awali Ruge amesem wananchi wa maeneo mbalimbali mkoani Mwanza wamefurahia na kunufaika kwa kupata huduma bora za afya,maji,umeme,elimu na barabara kutokana na utekelezaji wa programu ya TAKUKURU Rafiki.

“Programu hiyo inayolenga kutambua kero katika sekta ya huduma za jamii na miradi ya maendeleo katika sekta za maji,elimu,nishati ya umeme,afya,ardhi na barabara imekuwa na manufaa kwa wananchi katika uboreshaji wa huduma,”amesema.

Mkuu huyo wa TAKUKURU amesema katika kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu,manufaa mengi yamepatikana kupitia programu hiyo ya TAKUKURU Rafiki ikiwemo kutengenezwa kwa pampu ya maji na kuwezesha wananchi wa Kata ya Mahina wilayani Nyamagana,kupata huduma maji sasa.

Pia, Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ilitoa fedha kiasi cha miloni 60 za kukarabati shule ya msingi Nyakasungwa iliyokuwa na hali mbaya ya miundombinu ya madarasa kutokana na uchakavu.

Ruge amesema elimu ya namna bora ya kuboresha huduma imeendelea kutolewa kwa watumishi katika maeneo yao ya utendaji na wananchi kwa pamoja kuweza kuzuia vitendo vya rushwa maeneo huduma zinakopatikana.

Hivyo, katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2024 TAKUKURU Mwanza,imezifikia Kata 21 na kufanya vikao 21 na wananchi ambapo kero 147 ziliibuliwa ili zitafutie ufumbuzi na watoa huduma wa sekta mbalimbali.

Ruge alifafanua kuwa kero 18 kati ya hizo 147 zilipatiwa majawabu na nyingine zinaendelea kufanyiwa kazi na kuwataka wananchi kuwasiliana na ofisi yake kwa kutumia namba 113 ya dharura kutoa taarifa ya vitendo vya rushwa.