April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

LSF yakutana na wadau kutathmini programu ya upatikanaji haki nchini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

SHIRIKA la Legal Services Facility (LSF) ambalo linajishughulisha na kazi ya kukuza upatikanaji wa haki kwa raia wote nchini hususani wanawake kupitia uwezeshaji wa kisheria linaendesha mkutano wa siku mbili kwa mashirika wanufaika wake pamoja na wadau wake kutoka Tanzania bara na Zanzibar Jijini Dodoma.

Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Agness Mkawe akizungumza na wakurugenzi wa mashirika ya watoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na wasaidizi wa kisheria wakati wa mkutano wa siku mbili wa wadau wanufaika wa Shirika la Legal Services Facility (LSF) uliofanyika Jijini Dodoma kuanzia tarehe 20 – 21 Oktoba 2021 kwa lengo la kufanya tathimini ya utekelezaji wa programu ya upatikanaji wa haki nchini mwaka 2021.

Mkutano huu wa siku mbili ulioanza Oktoba 20 na 21 unajumuisha washiriki takribani 200 ikiwemo Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Watoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria kutoka mikoa yote nchini Tanzania.

Vilevile mkutano huu unajumuisha mashirika wanufaika wa mradi wa uwezeshaji kisheria katika maeneo ya mijini (Urban Legal Empowerment Grantees) pamoja na wadau wengine muhimu kutoka katika sekta ya msaada wa kisheria nchini Tanzania.

Mkutano huo umelenga hasa kutoa wigo wa kubadilishana taarifa kuhusu matokeo ya programu na kujadili pamoja kwa umuhimu na kimkakati mafanikio ya LSF kwa miaka ijayo zaidi baada ya mwaka 2021 kwa wanufaika na wadau wote wa LSF.

Hii inakuja kuelekea utekelezaji wa mpango mkakati mpya wa LSF wa miaka mitano ijayo unaotarajia kuanza mwakani 2022 mpaka 2026.

Mkutano huu umelenga kukuza ufanisi wa kiutendaji, utoaji wa huduma, ushirikishaji wa wananchi katika mifumo ya huduma za msaada wa kisheria kwa ajili ya kuchochea ukuaji na ustawi wa uwajibikaji, ushiriki na ujumuishwaji wa raia katika mifumo ya uwezeshaji wa kisheria nchini.

Kikubwa zaidi, katika mkutano huo, LSF pamoja na wadau wake wanalenga kujionea bayana pamoja na kujifunza kuhusu hali ya maendeleo na matokeo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na wanufaika wa LSF katika kipindi hiki cha mpito 2021 baada ya kumalizika kwa utekelezaji wa awamu ya pili ya program miaka mitano (2016 -2020) hapo Disemba 2020.
Vilevile, mkutano huo unalenga kutambua jitihada na juhudi za Wasaidizi wa Kisheria nchini waliowezeshwa moja kwa moja na LSF pamoja na kujadili malengo ya baadaye kuelekea utekelezaji wa mpango mkakati mpya wa 2022-2026.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huu Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria kutoka Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi, na Utawala Bora Visiwani Zanzibar, Hanifa Ramadhan Said amesema kuwa mkutano huo ni muhimu kwakuwa unawaleta pamoja wadau msaada wa kisheria ambao wamekuwa ni sehemu kubwa ya mafanikio katika kukuza upatikanaji wa haki nchini.

“Mkutano huu ni muhimu sana kwa wadau wa sekta ya msaada wa kisheria. Kumekuwa na taabu mbalimbali katika jamii ambazo husababishwa na ukandamizaji wa haki mbalimbali ikiwemo wanawake na Watoto. Kupitia programu ya LSF na wadau wake nchini mmeweza kufanya kazi kubwa ya kusaidia jamii kupitia uwezeshaji wa kisheria.”

Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Shirika la Legal Services Facility, Ezekiel Joachim, Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Tanzania bara, Agness Mkawe na Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria kutoka Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Hanifa Ramadhan Soud wakifuatilia mjadala kutoka kwa wadau wanufaika wa LSF wakati wa mkutano wa siku mbili uliofanyika Jijini Dodoma kwa ajili kufanya tathimini ya utekelezaji wa program ya upatikanaji wa haki nchini Tanzania mwaka 2021.

Amesema Hanifa.
Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Agness Mkawe amesema kuwa anaamini kuwa zoezi la tathmini ya utekelezaji wa program ya upatikanji wa haki nchini Tanzania litakwenda sambamba na wadau wote wa sekta ya msaada wa kisheria kuelekezana kuhusu kutii matakwa ya kisheria juu ya uendeshaji wa taasisi au mashirika yanatoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria nchini Tanzania.

“Kupitia mkutano huu ningependa kuwakumbusha kuendelea kutii sheria. Najua waliopo katika mkutano huu ni wakurugenzi ambao ndio watendaji wakuu wa taasisi zenu. Niwaombe kutii sheria zote kama inavyotakiwa.

Kuzingatia sheria zilizowekwa inarahisisha utendaji wenu kwakuwa inasaidia taasisi zenu kutambulika na mamlaka mbalimbali za kiserikali,” amesema Wakili Mkawe.

Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Agness Mkawe akizungumza na wakurugenzi wa mashirika ya watoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na wasaidizi wa kisheria wakati wa mkutano wa siku mbili wa wadau wanufaika wa Shirika la Legal Services Facility (LSF) uliofanyika Jijini Dodoma kuanzia tarehe 20 – 21 Oktoba 2021 kwa lengo la kufanya tathimini ya utekelezaji wa programu ya upatikanaji wa haki nchini mwaka 2021.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema kuwa amefurahi kukutana na wadau wake wote ambao amekuwa akifanya nao kazi nchi nzima, ambapo kwa kipindi cha miaka kumi wameweza kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuundwa kwa sheria ya msaada wa kisheria mwaka 2017.

“Nafurahi kukutana na wadau wetu wakubwa ambao mmekuwa mkifanya kazi kubwa ya kutekeleza program yetu ya upatikanaji haki nchi nzima. Naona fahari kuona kuwa LSF sasa imetimiza miaka 10 tangu ianze kutekeleza program yake na kupitia mashirika wanufaika wake tumefikia mfanikio mbalimbali ya sekta ya msaada wa kisheria. Naamini kuwa baada ya kikao hiki kazi yetu itaendelea kwa kasi zaidi ili kuwa na jamii iliyowezeshwa kisheria kupitia huduma bora za msaada wa kisheria,” amesema Lulu Ng’wanakilala.

Legal Services Facility (LSF) ni mfuko wa fedha ulioanzishwa mwaka 2011 kama shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki kwa wote, hasa wanawake kwa njia ya uwezeshaji wa kisheria. LSF hutoa fedha kwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa msaada wa kisheria na huduma za wasaidizi wa kisheria Tanzania bara na Zanzibar.

Kukuza na kulinda haki za binadamu kwa raia wote nchini hususani wanawake masikini, wasichana na makundi mengine yanyoweza kudhuriwa. Tunaongeza upatikanaji, unafuu na kukubalika kwa huduma za msaada wa kisheria kwa njia ya wasaidizi na watoaji wengine wa msaada wa kisheria.

LSF inafanya kazi karibu na serikali ya Tanzania katika ngazi zote, wabia wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoshiriki katika kutoa msaada wa kisheria zikiwemo, huduma za wasaidizi wa kisheria na wadau wengine wanaofanya kazi kama hiyo.

Baadhi ya Wakurugenzi wa mashirika ya watoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na wasaidizi wa kisheria wakifuatilia kwa umakini mada zinazotolewa na wawasilishaji mbalimbali kutoka Shirika la Legal Services Facility (LSF) wakati wa mkutano wa siku mbili wa wadau wanufaika wa LSF uliofanyika Jijini Dodoma kuanzia tarehe 20 – 21 Oktoba 2021 kwa lengo la kufanya tathimini ya utekelezaji wa programu ya upatikanaji wa haki nchini mwaka 2021.