Na Joyce Kasiki, Tanga
WADAU wa elimu nchini wametakiwa kubadili mifumo ya elimu, mitaala na namna ya kufundisha ili kuandaa wahitimu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia, ikiwa Tanzania inataka kutimiza malengo ya maendeleo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa 2050.
Wito huo umetolewa leo Agosti 19 2026 na Mshauri wa masuala ya Elimu Kimataifa Mhandisi Henry Kulaya wakati akizungumza katika Kongamano la Elimu lkuhusu “Mageuzi ya Elimu ya Juu na Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Maendeleo Endelevu, Ujuzi, Ubunifu na Ushindani wa Kiuchumi Kuelekea Dira ya Taifa 2050,” lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga.
Kulaya amesema kasi ya mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya kazi inalazimisha taasisi za elimu ya juu pamoja na elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kufanya mageuzi makubwa, badala ya kuendelea kutumia mifumo iliyojengwa kwa kuzingatia mahitaji ya zamani.
Amesema Dira ya Taifa 2050 ni azma kubwa inayohitaji ushiriki wa kila kizazi, huku taasisi za elimu zikiwa na jukumu la msingi katika kuandaa rasilimali watu watakaoweza kutatua changamoto, kutumia fursa na kuleta suluhisho zinazotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
“Hatuzungumzii teknolojia pekee,tunazungumzia namna ya kufikiri tofauti, namna ya kujifunza na namna ya kushirikiana katika mazingira yanayobadilika,” amesema.
Amesema maendeleo ya teknolojia yamebadili kwa kasi namna watu wanavyoishi, kufanya kazi na kujifunza, hivyo taasisi za elimu haziwezi tena kujikita katika kuwapa wanafunzi taarifa pekee.
Kwa mujibu wa Kulaya, dunia imepitia hatua mbalimbali za mapinduzi ya viwanda, kuanzia matumizi ya mitambo ya mvuke, uzalishaji kwa wingi, matumizi ya kompyuta na mifumo ya kiotomatiki, hadi mifumo mtandao, intaneti ya vitu na sasa ushirikiano kati ya binadamu na mashine.
Amesema kasi ya mabadiliko hayo imeongezeka kwa kiwango kikubwa, jambo linaloifanya elimu kuhitaji kubadilika sambamba na mahitaji mapya ya jamii na soko la ajira.
“Swali si kwamba tunafundisha nini tu, bali tunawaandaa watu wa aina gani kwa dunia inayobadilika kwa kasi,” amesema.
Amesema kizazi cha sasa kinaishi katika mazingira ambayo taarifa zinapatikana kwa urahisi, hivyo elimu inapaswa kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuchambua taarifa, kufikiri kwa kina, kuwasiliana, kushirikiana na kutengeneza suluhisho bunifu.
Kulaya ameonya kuwa kuendelea kupima mafanikio ya elimu kwa vyeti na sifa za kitaaluma pekee kunaweza kushindwa kukidhi mahitaji ya soko la ajira na uchumi wa kisasa.
Amesema badala yake, elimu inapaswa kujikita katika uwezo wa mhitimu kutumia maarifa kutatua matatizo halisi, kubuni bidhaa na huduma, kuanzisha shughuli za kiuchumi na kukabiliana na mazingira yenye changamoto na yasiyotabirika.
Aidha, amesema taasisi za elimu zinapaswa kuacha mtazamo wa kushikilia mifumo ya zamani kwa sababu tu imekuwa ikitumika kwa muda mrefu, na badala yake ziwe tayari kuhoji mifumo iliyopo na kujaribu mbinu mpya za ufundishaji na ujifunzaji.
“Tunapaswa kufikiria upya namna tunavyofundisha, namna tunavyojifunza na namna tunavyotatua matatizo,dunia haibaki pale ilipokuwa jana,” amesema.
Kulaya pia amesisitiza umuhimu wa utafiti na ubunifu katika kuandaa Tanzania kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo, akisema sayansi na teknolojia vinapaswa kutumika kama nyenzo za kutengeneza suluhisho na si kuwa lengo lenyewe.
Amesema mabadiliko hayo yanahitaji ushirikiano wa vizazi mbalimbali, kwa kuwa dunia ya sasa inawakutanisha watu wenye uzoefu wa vizazi tofauti na teknolojia mpya inayotumiwa zaidi na vijana.
“Tunapaswa kujenga mazingira ambayo vizazi mbalimbali vinaweza kujifunza kutoka kwa kila mmoja, kushirikiana na kuleta mawazo mapya,” amesema.
Amesema mazingira ya sasa yana changamoto nyingi, ambazo haziwezi kutatuliwa kwa kutumia jibu moja au njia zilizotumika zamani, hivyo wataalamu wanahitaji kuwa na uwezo wa kubadilika, kujifunza upya na kubuni njia mbadala.
Kwa upande wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, amesema sekta hiyo ina nafasi kubwa katika kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi unaohitajika katika uchumi unaobadilika, hususan katika teknolojia, viwanda na sekta nyingine zinazohitaji wataalamu wenye uwezo wa vitendo.
Amesema kuelekea Dira ya Taifa 2050, Tanzania inahitaji mfumo wa elimu unaozalisha wahitimu wanaoweza kuingia katika ajira wakiwa tayari kukabiliana na mahitaji halisi ya dunia ya kazi, lakini pia wenye uwezo wa kujiajiri na kuanzisha shughuli za kiuchumi.

More Stories
Sound Beat and Soft yazindua duka la vifaa vya muziki Kariakoo
Ocean Road yatoa wito waishio vijijini kupuuza mila potofu
Kutoka Maabara hadi Sokoni: UDSM yabuni Saruji na Teknolojia rahisi za Ujenzi