Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
KAMPUNI ya Barrick inayoendesha shughuli zake nchini kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals imesema uwekezaji wake nchini umeanza kuonyesha namna utajiri wa madini unavyoweza kuchangia mapato ya serikali, Pato la Taifa (GDP) , ajira kwa watanzania, fursa kwa biashara za ndani na jinsi inavyotengeneza mazingira ya kuwaandaa wataalamu kwa ajili ya uchumi wa baadaye kwendana na mkakati wa serikali ya Tanzania ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza katika mkutano wa Wakurugenzi Wakuu wa Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum) 2026 unaofanyika Arusha, Meneja Rasilimali Watu wa Barrick nchini, Lumbu Kambula alisema uwekezaji wa kampuni hiyo unaendelea kugusa maeneo yanayolengwa katika Dira 2050, ikiwamo ajira,ukuzaji wa biashara za ndani, ujuzi, elimu na uwekezaji wa muda mrefu na kuhakikisha utajiri wa rasilimali za nchi unazalisha manufaa yanayoonekana kwa serikali na watanzania.
“Barrick-Twiga ni mshirika anayetoa thamani endelevu kwa Tanzania na tunaendelea kutoa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na mwekezaji wa kimataifa uliojengwa juu ya thamani ya pamoja katika uchimbaji madini na tunawajibika kwa maendeleo ya taifa,” amesema Kambula.

Amesema tangu mwaka 2019, ubia kati ya Serikali na Barrick umeonyesha namna uwekezaji katika sekta ya madini unavyoweza kuleta mafanikio ya kibiashara huku ukitoa thamani kwa Serikali, wafanyakazi, biashara za Kitanzania, jamii zinazozunguka migodi na wanahisa.
Kambula amesema asilimia 93 ya matumizi ya kampuni hiyo kwa sasa yanaelekezwa kwa wazabuni wa ndani, huku matumizi kwa kampuni zinazomilikiwa na Watanzania yakifikia asilimia 79, kutoka asilimia 34 mwaka 2019.
Amesema zaidi ya trilioni 12 zimewekezwa nchini na kulipwa kwa Serikali ya Tanzania.
“Barrick Twiga inasaidia kubadilisha utajiri wa madini tulionao kuwa mapato ya Serikali, shughuli za kiuchumi, ajira, fursa kwa biashara za ndani na uwekezaji wa muda mrefu,” amesema

Katika eneo la ajira, Kambula amesema asilimia 95 ya wafanyakazi wa Barrick ni Watanzania, huku wakiendelea kushika nafasi za kitaalamu, kiufundi na uongozi ambapo pia kampuni inaendelea kuwekeza katika kuandaa kizazi cha wataalamu wa sekta ya madini kupitia programu za mafunzo kwa vitendo.
“Kwa upande wa mafunzo na kuandaa wataalamu katika nyanja mbalimbali,Barrick ina mipango mbalimbali ya kupokea na kufundisha wanafunzi wa vyuo na zaidi ya wahitimu 50 kila mwaka wanapata nafasi ya kujiunga na mafunzo ya vitendo kwa kipindi cha miaka miwili katika migodi yetu,”alisema.
“Pia zaidi ya wanafunzi 250 kutoka vyuo vikuu na vya ufundi wanapata nafasi za kufanya mafunzo kwa vitendo kila mwaka. Hii inaonyesja jinsi gani Barrick inaendana na maagizo ya Makamu wa Rais , Deogratias Ndejembi ya kuandaa na kutoa nafasi kwa vijana wetu kupata uzoefu wakati wakijiandaa kuingia katika soko la ajira,”amesema

Amesema mwaka 2025 kampuni ilianzisha mpango wa ufadhili wa wanafunzi wa kitanzania kwenda kusoma nje nchini Afrika Kusini, ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa wataalamu kwa soko shindani la ajira.
Kambula pia kampuni kwa kushirikiana na Serikali inatekeleza mradi wa kimkakati wa Barrick-Twiga Future Forward Education Program ukiwa unalenga kuboresha miundombinu ya shule za sekondari za serikali nchini mradi ambao utagharimu takribani shilingi bilioni 70.5.
Mradi huu umelenga kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 1,090,majengo ya maliwato na vyoo 1,660 na mabweni 270 katika shule 161 nchini kote ambapo katika awamu ya kwanza mradi umefanikisha kujenga madarasa ya kisasa 374,mabweni ya kisasa 89 na mashimo ya vyoo na maliwato 569.
Amesema hatua hizo ni sehemu ya uwekezaji katika rasilimali watu ambao ni muhimu katika maandalizi ya Tanzania kuelekea uchumi unaolengwa na Dira 2050.
Amesema kampuni hiyo pia imeendelea kuwekeza katika kutafuta rasilimali mpya za madini.
Kambula amesema Barrick imewekeza dola za Marekani milioni 33.5 katika utafiti wa madini, ikiwa na lengo la kugundua rasilimali mpya nchini.
Amesema uwekezaji wa kampuni hiyo umevuka shughuli za migodi, ambapo dola za Marekani milioni 16.3 zimetumika katika miradi ya kijamii, ikiwamo ujenzi wa barabara ya Kahama-Kakola yenye urefu wa kilomita 73 kwa kiwango cha lami.

More Stories
GCLA yasisitiza udhibiti salama wa kemikali migodini
Umoja Afya ya NHIF yawavutia wengi Geita
Kurudi Shuleni baada ya Ujauzito,Safari yenye Miiba