Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
Wadau wa muziki, wasanii na wapenzi wa burudani wamekaribishwa kutumia fursa ya duka jipya la Sound Beat and Soft, lililopo Kariakoo, Mtaa wa Lindi, Dar es Salaam, ambalo limezinduliwa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya muziki kwa wasanii na wadau wa sekta hiyo.
Duka hilo limekuja wakati ambapo sekta ya muziki nchini ikiendelea kukua na mahitaji ya vifaa bora vya kurekodia, kutengeneza na kuwasilisha muziki yakiongezeka.
Sound Beat and Soft limejipambanua kwa kuwa na vifaa mbalimbali vinavyolenga kukidhi mahitaji ya wasanii, waimbaji, waandaaji wa muziki pamoja na watu wanaofanya shughuli za burudani na matukio.
Akizungumza katika uzinduzi huo, msanii wa muziki Nyoshi El Saadat aliipongeza Beat Sounds and Soft kwa uamuzi wa kuwekeza katika biashara ya vifaa vya muziki, akisema uwepo wa duka hilo ni hatua nzuri kwa sababu unawapa wasanii na wadau wa muziki sehemu ambayo wanaweza kupata vifaa kwa urahisi.

Nyoshi alisema ubora wa vifaa ni jambo muhimu katika kuhakikisha kazi za wasanii zinafanyika kwa kiwango kinachokubalika, hivyo uwepo wa sehemu yenye vifaa mbalimbali ni fursa kwa tasnia nzima ya muziki.
“Nimefurahi kuona duka kama hili limefunguliwa hapa Kariakoo. Kitu kizuri nilichokiona ni kwamba kuna vifaa vingi na vya aina mbalimbali ambavyo msanii au mtu anayehusika na muziki anaweza kuhitaji. Hii ni hatua nzuri kwa sababu inarahisisha upatikanaji wa vifaa na inawapa wasanii nafasi ya kuchagua kile kinachowafaa,” alisema Nyoshi.

Aliongeza kuwa Beat Sounds and Soft haipaswi kuonekana kama sehemu ya biashara pekee, bali pia kama sehemu inayoweza kuchangia maendeleo ya vipaji na ubunifu nchini kwa kuwa wasanii wanahitaji mazingira mazuri pamoja na vifaa vinavyowawezesha kuzalisha kazi zenye ubora.
“Muziki wa sasa unahitaji vifaa vizuri. Huwezi kutaka msanii afanye kazi nzuri bila kumpa mazingira na vifaa vinavyomsaidia kufikia kiwango anachokitaka. Kwa hiyo, uwepo wa Beat Sounds and Soft ni jambo la kupongeza na ninaamini wadau wengi watapata msaada kupitia duka hili,” alisema.
Kwa upande wake, msanii wa vichekesho Stan Bakora aliipongeza biashara hiyo akisema amevutiwa na namna duka hilo lilivyoandaliwa pamoja na aina mbalimbali za vifaa vinavyopatikana ndani yake.
Stan alisema uwekezaji katika vifaa vya muziki una umuhimu mkubwa kwa wasanii na waandaaji wa burudani, akibainisha kuwa sekta ya burudani inahitaji wafanyabiashara wanaoamini katika vipaji vya Watanzania na kuweka bidhaa zinazoweza kusaidia kazi zao.
Naye Benedict Lugai, Meneja Sound Beat ameeleza kuwa uwepo wa Beat Sounds and Soft ni hatua inayoweza kusaidia kukuza mazingira ya uzalishaji wa muziki na burudani nchini, hasa kwa kuwa wasanii wanahitaji upatikanaji rahisi wa vifaa ili kuendeleza kazi zao na kufikia viwango vya juu zaidi.

More Stories
Ocean Road yatoa wito waishio vijijini kupuuza mila potofu
Kutoka Maabara hadi Sokoni: UDSM yabuni Saruji na Teknolojia rahisi za Ujenzi
Tanga kujiandaa kupokea Gesi Asilia kwa matumizi