April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jumuiya ya Maridhiano yatekeleza agizo la serikali

Na Rose Itono,Timesmajira, Online

JUMUIYA ya Maridhiano Tanzania imefanya mabadiliko ya katiba yake kama ilivyoagizwa na serikali na kufanya uchaguzi wa viongozi wapya watakoongoza kwa miaka mitano ambapo Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa jumuiya hiyo

Amesema mbali na Shekhe Alhad Mussa Salum, kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Taifa pia imemchagua, Dkt. Elias Silayo kuwa Makamu Mwenyekiti Taifa.

Mkutano huo umemuachisha uongozi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Mchungaji Osward Mlay na kumfukuza kabisa uanachama huku ikithibitisha majina kumi ya wadhamini waliopendekezwa na Kamati Kuu.

Akisoma taarifa ya maazimio yaliyopitishwa kupitia Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Shekhe Abdulrazak Amri Juma alisema Mkutano Mkuu umefanya mabadiliko ya katiba kama ilivyoagizwa na msajili.

Ameyataja baadhi ya majina kumi yaliyopitishwa na Kamati Kuu kuwa ni pamoja na Gaudence Lyimo, Shekhe khamis Mataka, Salum Muhsin, Lazaro Mambosasa na Suleyman Kova.

Wengine ni Philip Mpango, Jaji Francis Mutungi, Azim Dewji na Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Akson.

“Kamati Kuu pia imewateua viongozi kadhaa wa kitaifa na viongozi wa mikoa, ambao kwa panoja watatakiwa kuhakikisha jumuiya hiyo inaendeleza malengo yake makuu ya kuendeleza amani ya nchi, sambamba na kuunga mkono serikali juu ya juhudi zake za kuwapatia Watanzania chanjo ya Corona iliyo salaam,” amesema Shekhe Amri.

Amesema Jumuiya, itamshughulikia kila mwanachama na kiongozi asiye na maadili na kukiuka Katiba ya Jumuiya hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo Taifa, Shekhe Alhad Mussa Salum amesema atahakikisha kipindi chake chote cha miaka mitano ya uongozi kikatiba, jumuiya hiyo inaendelea kushirikiana na taasisi zote zenye nia na dhamira njema kwa Watanzania wote.

Hivi karibuni baada ya Rais, Samia Suluhu Hassan kuzindua rasmi chanjo ya Corona viwanja vya Ikulu ya Jijini Dar es Salaam na kuchanja Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, iliunga mkono hatua hiyo kwa kusema wajumbe wake wako tayari kuchanja ili kuwa mfano kwa Watanzania wengine katika kupiga vita ugonjwa huo, zoezi ambalo pia lilienda sambamba na uchanjaji kwenye viwanja vya Karimjee.