April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Global Education Link yawataka wanafunzi wanaosoma nje ya nchi kutangaza Utalii

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WAKALA wa elimu nje ya nchi Global Education Link (GEL) imewataka Wanafunzi watakaokwenda nje ya nchi kwaajili ya masomo kuitangaza Tanzania ili kuongeza watalii na wawekezaji nchini.

Hayo aliyasema jana Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Education Link, Abdulmalik Mollel wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam katika Maonesho ya 17 ya Vyuo Vikuu yanayoendelea katika viwanja vya mnazi mmoja,

“Tunamuona mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan anavyokwenda nje na kulitangaza Taifa letu na fursa tulizonazo na uzuri wa nchi yetu, hivyo tuendelee kuvutia wawekezaji na watalii nchini,” alisema.

Kwa upande mwingine, Mollel alisema Global Education Link wameandaa mahafali ya wanafunzi wa Tanzania waliofanikiwa kumaliza elimu yao nje ya nchi ambayo yatakuwa ni mahafali ya tatu tangu kuanza kwake mwaka 2019 yatakayofanyika tarehe 21/8/2022 Mlimani city jijini Dar es salaam.

Mollel aliwataja watu watakaoshiriki katika mahafali hayo kuwa ni pamoja na mgeni rasmi, mabalozi ambao ni watanzania wanaosoma nje ya nchi na wanafunzi mbalimbali na wazazi.

Aidha Mollel amesema anayeruhusiwa kushiriki mahafali hayo ni yule aliyehitimu na mwenye uthibitisho kuwa amehitimu akiwa na cheti cha kuhitimu kutoka chuo kikuu.

Mbali na hayo Mollel alizitaja Changamoto zinazowapelekea baadhi ya wanafunzi wanapokuwa nje kushindwa kufikia hatua ya kuhitimu ikiwa ni pamoja na mzazi kushindwa kulipa ada kwa wakati kutokana na miongozo ya chuo inavyotaka.