April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aweso: Pangeni ratiba rafiki mgao wa maji katika kipindi hiki cha mpito

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Kufuatia changamoto ya upatikanaji wa maji kwa baadhi ya maeneo jijini Mwanza hususani yenye miinuko kutokana na kuharibika kwa mitambo ya kusukuma maji katika kituo cha mabatini.

Waziri wa Maji, Juma Aweso ameiagiza Bodi ya Maji ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Mwanza (MWAUWASA) na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo kupanga ratiba rafiki ya mgao wa maji ili kuwawezesha wananchi waishio maeneo ya miinuko kupata maji.

Aweso ameeleza hayo baada ya kutembelea mitambo ya kusukuma maji Mabatini ili kuangalia hitlafu iliotokea ya mota mbili kuungua na hivyo kuathiri na kushusha uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 90 hadi lita milioni 80 kwa siku.

Ameeleza kuwa hitlafu iliyotokea katika mitambo hiyo ya kusukuma maji imewathiri zaidi wananchi wanaoishi katika maeneo ya miinuko kwa kukosa huduma ya maji hivyo kuiagiza bodi na uongozi wa MWAUWASA kuweka mgawo wa haki sawa katika maeneo hayo wapate huduma.

“Nimeridhika kwa namna wataalamu na watendaji wanavyojitahidi kufanya ukarabati kurejesha kiwango cha uzalishaji maji kwa sababu hitlafu iliyotokea imesababisha upungufu wa lita milioni 10 za maji, wananchi wanaoishikatika miinuko hawana huduma ya maji.Naagiza Bodi na Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA kuweka ratiba maalumu ya mgawo wa maji,”ameeleza Awesso.

Pia ameeleza kuwa Rais Samia hataki kusikia taharuki ya maji kwa wananchi hivyo Wizara na MWAUWASA itahakikisha changamoto hiyo inakwisha na kuwaomba wananchi wa Jiji la Mwanza wawe watulivu ambapo wizara itahakikisha mitambo inaimarishwa kwa kuikarabati ili kurejesha kiwango cha maji.

Aidha ameeleza kuwa watalamu wa MWAUWASA hawalali wanahangaika kuhakikisha changamoto hiyo inakwisha ili wananchi wanaoishi katika miinuko wanapate huduma ya maji kwa usawa.

“Sitakubali mgawo wa maji wa upendeleo,nahitaji kuona wananchi wa kwenye miinuko wanapata huduma ya maji kwa ubora na kwa wakati,kwa sababu ya hitalafu iliyotokea katika mitambo, hatuwezi kukubali wananchi wakose maji hasa katika miiunko, wekeni ratiba maalum maana maji hayana mbadala ,wananchi wakikosa maji hayo maisha yao yanakuwa hatarini,”ameeleaa Aweso.

Muonekano wa kituo cha maji safi Mabatini ambacho ilitokea hitilafu ya mota mbili za kusukumia maji kuungua na kusababisha changamoto ya upatikanaji wa maji kwa baadhi ya maeneo ya Jiji la Mwanza hususani maeneo ya miinuko.(Picha na Judith Ferdinand)
Mkurugenzi wa MWAUWASA Mhandisi Leonard Msenyele akitoa maelekezo kwa Waziri wa Maji Juma Aweso alipotembelea kituo cha maji safi Mabatini ili kujionea hali halisi ya hitilafu ilitokea ya mota mbili za kusukumia maji kuungua.(Picha na Judith Ferdinand)