Na Joyce Kasiki Timesmajira online,Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burhan, amewataka wananchi wa mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kutembelea maonesho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga.
Akizungumza leo Agisti 17,2026 na waandishi wa habari katika maonyesho hayo, Balozi Burhan amesema maonesho hayo ni fursa kwa wananchi kujifunza na kuona bunifu mbalimbali zinazolenga kuchochea maendeleo ya Taifa.
Amesema Serikali ya Mkoa wa Tanga itaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha maonesho hayo yanafanyika kwa usalama na kuwafikia wananchi wengi, huku akipongeza maandalizi yaliyofanywa na waandaaji.
Maonesho hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa 2050,” ikiwa ni mkakati wa kuwaandaa Watanzania wenye elimu, ujuzi na uwezo wa kubuni suluhisho zitakazosaidia kufikia malengo ya Dira hiyo.
Balozi Burhan pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji katika sekta ya elimu, akisema Serikali imetenga takribani Sh bilioni 156 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Amesema maonesho hayo, yanayofanyika kwa mara ya pili, yamewakutanisha zaidi ya washiriki 300 kutoka vyuo vikuu, taasisi za utafiti na maendeleo, vyuo vya ualimu, taasisi za elimu na mafunzo ya ufundi na stadi pamoja na taasisi binafsi.
Mkuu huyo wa Mkoa amewahimiza wananchi wa Tanga, mikoa jirani na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ili kujifunza na kuona bunifu zinazolenga kuimarisha elimu, ujuzi na teknolojia nchini.

More Stories
WiNTz yawafungulia fursa wanawake KCMC teknolojia ya nyuklia
Katibu Mwenezi Wilaya ya Mkuranga Omari Kisatu atoa maelekezo mazito
Masandawana Fc yajinyakulia mil.10/- Tulia Trust Uyole Cup 2026