August 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mwenezi Wilaya ya Mkuranga Omari Kisatu atoa maelekezo mazito

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

KATIBU Mwenezi Wilaya ya Mkuranga Omari Kisatu amewataka wazazi na walez nchini kujenga tabia ya kushirikiana na walimu katika malezi ya watoto ili kuwa na kizazi bora

Kisatu ameyasema hayo leo kwenye mahafali ya tano ya darasa la Saba Shule ya Msingi Juhudi iliyopo Kata ya Mwandege Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani ambapo alimwakilisha Mbunge wa Jimbo hilo na Waziri wa Ujenzi Abdalah Ulega

Amesema tabia ya kuwaachia walimu peke yao kwenye malezi ya watoto inawapa mzigo mkubwa walimu na hatimaye kuzalisha kizazi kisicho na maadili

” Wazazi walezi tushirikiane kwa pamoja katika kuhakikisha watoto wanakuwa kwenye misingi inayofaa kwa faida ya kizazi kijacho yetu na taifa kwa ujumla, ” amesema Kisatu

Amesema kila mzazi na mlezi ana wajibu wa kumfuatilia mtoto wake ili kujua maendeleo yake shuleni badala ya kuwaachia walimu peke yao

Pia alikabidhi kwa uongozi wa shule hiyo pesa taslimu kiasi cha sh.milioni mbili kwa ajili ya kuanza kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili shule

Awali Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Makarius Kihawa
kwenye risala yake imeiomba serikali na wadau mbalimbali kuwajengea uzio ili kulinda usalama wa wanafunzi wa shule hiyo

Amesema wanafunzi wa shule hiyo wanasona katika mazingira magumu kutokana na kuwepo kwa muingiliano wa makazi ya watu hivyo
kukosekana kwa uzio kunawaweka wanafunzi kwenye mazingira magumu ya ujifunzaji

“Shule yetu inakabiliwa na muingiliano wa jamii hususan muda wa vipindi bodaboda na watu mbalimbali wamekuwa wakipita pembezoni mwa madarasa ya shule na kusababisha kutokuwepo kwa umakini wa wanafunzi darasani ” amesema Mwl. Kihawa

Amesema shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 2,000 wakiwepo wenye mahitaji maalumu mbali ya kuwa na changamoto ya uzio pia inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya nadarasa na vitendea kazi mbalimbali

“Awali shule ilipoanzishwa na kusajiliwa mwaka 2019 ilikuwa na idadi ya wanafunzi 788 lakini kwa sasa kuna jumla ya wanafunzi imeingezeka na kufikia 2,385 huku ikiwa na idadi ya vyumba 12 vya madarasa na uhitaji ni vyumba 59, ” amesema Mwl. Kihawa

Aidha ameongeza kuwa walimu wa shule hiyo wamekuwa na jitihada ya kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza darasa la saba shuleni hapo wanafaulu vizuri na kwamba ufaulu umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka

Kwa upande wake Mwenyekiti wa shule hiyo Zainab Mtandika amesema muingiliano wa shughuli mbalimbali za kijamii zikiwepo bodaboda zinazopita mara kwa mara shuleni hapo zinatilia waswasii mkubwa wa usalama wa wanafunzi hasa kwa watoto wa kike

” Mbali ya shule yetu kuwa na muingiliano na jamii pia Kuna shule jirani ambayo ni ya sekondari ambayo Ina wanafunzi wa kiume hali inayowapa ugumu walimu kusimamia ulinzi wa wanafunzi wa kike muda wote,” amesema Mtandika na kuongeza shule hiyo pia ina wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambao wanahitaji kusimamiwa kwa karibu

Amesema kwa mwaka 2026 wanafunzi watafaulu kwa ufaulu wa zaidi ya asilimia 100 kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanywa na walimu

” Mwaka 2022 ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba kwenye mtihani wa Taifa ulikuwa ni asilinia 91.7, mwaka 2023 ilongezeka na kuwa asilimia 93, 2024 ilikuwa asilimia 96, 2025 ilikuwa asilimia 98.8 ambapo kwa mwaka huu wa 2026 tumejipanga kuvunja rekodi kwa kuwa na ufaulu wa zaidi ya asilimia 100

Jumla ya wanafunzi 257 wanatarajia kufanya mtihani wa Taifa wa kumaliza elimu ya msingi shuleni hapo hivi karibuni