March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Elimu ya hifadhi ya jamii yavutia wengi Maonesho ya Sabasaba

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online

WAKATI Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam yakiendelea, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii, kutatua kero mbalimbali za wanachama na wadau waliotembelea banda hilo.

Mmoja ya wanachama aliyetembelea banda la NSSF, Bahiru Gwimile, amesema alijiunga na NSSF kupitia sekta isiyo rasmi akawa anajiwekea akiba kila mwezi, lakini baadaye alipata kazi ambapo aliendelea kuitumia akaunti yake ile ile mpaka mkataba wake wa ajira ulipomalizika na sasa ameamua kujichangia tena kupitia sekta isiyo rasmi.

Rehema Lugome ambaye ni Afisa Huduma kwa Wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), akitoa huduma kwa mwanachama aliyetembelea banda namba 13 katika maonesho ya SabaSaba, jana.

“Nahamasisha vijana wenzangu, makundi mbalimbali na watu wote ambao hawajajiunga na NSSF wajiunge kwa sababu unapojiwekea akiba NSSF kuna faida ambazo utanufaika nazo baadaye kama kupata pensheni ya uzeeni ambayo itakufanya ufurahie maisha mazuri ya uzee wako,” amesema.

Afisa Mwandamizi Tehama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Rukia Zuberi, akimuhudumia mwanachama aliyefika kwa ajili ya kuangalia taarifa za michango yake. NSSF ipo katika banda namba 13 maonesho ya SabaSaba.

Kwa upande wake, Afisa Mafao Mwandamizi wa NSSF, Stella Kabyemera, amesema NSSF ilianza kutoa huduma kwa wanachama na wadau katika maonesho hayo yaliyobeba kauli mbiu isemayo “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu” kuanzia Juni 28,2021 na wataendelea kutoa huduma mpaka Julai 13, mwaka huu, katika banda namba 13 la mashirikiano baina ya PSSSF na NSSF.

.Afisa Mafao Mwandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Stella Kabyemera, akitatua kero za mwanachama aliyefika katika banda la NSSF namba 13, jUzi katika maonesho ya SabaSaba.

“NSSF kupitia maonesho haya inatoa elimu ya hifadhi ya jamii, inatatua kero mbalimbali kuhusu mafao, baadhi ya wanachama wamepata huduma ya kuangalia taarifa za michango yao na kwa wale wanachama ambao hawajapata kadi zao za uanachama tunawaomba watembelee banda letu ili waweze kupata kadi zao.”

Mkaguzi Mwandamizi wa NSSF, Revocatus Kiduli, akimuonesha mwanachama wa NSSF taarifa za michango yake, alipotembelea banda namba 13 katika maonesho ya SabaSaba.

NSSF inatoa huduma zake zote zinazopatikana kwenye ofisi zake mbalimbali nchi mzima, pia wanatoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi kama wajasiriamali, wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo, mama lishe na bodaboda.