




Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MKUU wa Tawi la Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Hassan Mabena, amesema JKT ni miongoni mwa wadau muhimu katika kuhakikisha mazingira yanakuwa salama kupitia matumizi ya nishati safi.
Aidha amelipongeza Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) limekuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kupitia matumizi ya nishati safi.
Brigedia Jenerali Mabena ameyasema hayo Juni 6,2026 Jijini Dodoma alipotembelea katika banda la TPDC kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani na kujionea magari yanayitunia gesi asilia badala ya mafuta.
Amesema jeshi hilo linaendelea kutoa mafunzo kwa vijana katika kambi mbalimbali nchini, ambapo kwa sasa linatarajia kuwa na zaidi ya vijana 70,000 na wanatumia nishati safi ya kupikia katika makambi yao.
Kuhusu TPDC amesema shirika hilo limekuwa likifanya juhudi zake za kugundua, kuchakata na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia inayopatikana nchini Tanzania.
“Nimejionea mfano wa gari linalotumia gesi asilia, na nishati hii ina mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira,” amesema.
Amefafanua kuwa nishati nyingi zinazotumika kwa sasa huzalisha moshi unaochangia uharibifu wa mazingira, tofauti na gesi asilia ambayo ni rafiki kwa mazingira huku akisema kuwa matumizi ya gesi asilia yana gharama nafuu, hivyo kumwezesha Mtanzania wa kawaida kuimudu.
Brigedia Jenerali Mabena amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inalenga kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya kijani kupitia uhifadhi wa mazingira, upandaji miti na matumizi ya nishati safi.
Pia amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuongoza katika masuala ya uhifadhi wa mazingira ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pamoja na Bara la Afrika kwa ujumla.
“Kwa mfano, nikiwa hapa katika banda la TPDC, naweza kusema kuwa ni miongoni mwa wadau wakubwa wanaochangia kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa salama kupitia matumizi ya nishati safi,” amesema.
Aidha amewataka wadau mbalimbali na Watanzania kwa ujumla kuendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuhifadhi mazingira ili kufanikisha azma ya kuwa na Tanzania ya kijani ifikapo mwaka 2030 na 2050.

More Stories
Uchorongaji visima vya gesi Mgawara neema kwa Wananchi
Tucta kuzindua kituo cha msaada kwa wafanyakazi wahamiaji Juni 11
Wanasiasa washauriwa kujikita kwenye masuala ya maendeleo